NA BEATUS MAGANJA
KUFUATIA changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu nchini, wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa hususani Shinyanga na Mwanza wamekubali na kuahidi kushirikiana na Serikali kukabiliana changamoto hiyo ili kupunguza adha kwa wananchi hasa wale wanaoishi pembezoni mwa hifadhi.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika ziara iliyofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania -TAWA katika Mikoa ya Kanda ya ziwa, wananchi hao wameelezea adha kubwa wanayoipata kutokana na changamoto itokanayo na wanyamapori hao kiasi cha kuhatarisha maisha yao na kudhoofisha shughuli za kiuchumi huku wakiipongeza TAWA kwa hatua yao ya kuwashirikisha wananchi katika zoezi zima la kukabiliana na changamoto hiyo.
"Kumekuwa na malalamiko makubwa sana kutokana na wimbi la wanyamapori hatarishi hususani fisi na wengine ambao wamekuwa wakishambulia watu, watoto wanashindwa hata kwenda shule, jambo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa" ameeleza Leonard Mayala mkazi wa Kahama
"Lakini ujio wa taasisi hii ya TAWA umekuwa ni faraja kubwa kwetu maana imekuja kwa ajili ya kushirikiana na wananchi ili kukabiliana na changamoto hii ya wanyamapori,..na mimi niseme, sisi kama wananchi tuko tayari kushirikiana na taasisi hii kwa sababu usalama ni wakwetu na taasisi hii imekuja na huu mpango kwa ajili ya kutuweka salama kwahiyo sisi wananchi tunaahidi kutoa ushirikiano kwa Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori hao," ameongeza.
Naye Robert Wilson mkazi wa wilaya ya Misungwi Kata ya Mbarika ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikundi cha wagalu ameeleza kufurahishwa kwake na adhma ya Serikali kupitia TAWA ya kuwashirikisha wananchi katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu na kuahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika mapambano hayo ili jamii iwe na amani.


Aidha ametoa rai kwa watanzania wote kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo ikizingatiwa kuwa jukumu la kulinda raia na mali zao ni la wananchi wote.