ARUSHA-Mkurugenzi wa Huduma za Posta Bw. Arubee Ngaruka amewaasa wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania kuyaishi mabadiliko ya kiutendaji yanayoendelea sasa ikihusisha maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ili kuendelea kukidhi mahitaji ya wateja.
Ameyasema hayo Mei 1, 2024 kwa niaba ya Postamasta Mkuu Bw. Maharage Chande wakati wa hafla fupi ya kumpongeza mfanyakazi hodari kitaifa sambamba na wafanyakazi wengine hodari kimkoa mara baada ya shughuli za Mei Mosi Kitaifa kukamilika jijini Ausha.
Akizungumza kwa niaba ya Postamasta Mkuu, Bw. Ngaruka ameeleza kuwa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kiutendaji wafanyakazi wanapaswa kuwajibika kwa nafasi zao na kuongeza juhudi katika utendaji ili kuongeza mapato ya ndani pamoja na kulifanya Shirika lilete tija kwa Taifa.
Ikumbukwe pia hivi karibuni Shirika la Posta Tanzania limezindua kauli mbiu yake mpya ijulikanayo kama “Posta Delivers Better” huku Bw. Arubee akiwasisitiza wafanyakazi kuhakikisha wanatoa huduma bora kuendana na mabadiliko mbalimbali yanayoendelea ndani ya shirika.
Wafanyakazi hodari kwa Shirika la Posta walikuwa ni Bw. Khamis Ame Mohamed ambaye ni Mfanyakazi Hodari kitaifa, Ziada Mbuyabuye Mfanyakazi Hodari mkoa wa Arusha pamoja na Veronica Magoto mfanyakazi hodari Mkoa wa Kilimanjaro.