Wanaoliza wastaafu mwisho wao wakaribia, Wastaafu Portal inakuja

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha imesema, inatarajia kuanzisha Mfumo wa Wastaafu Portal ambao unalenga kuwaokoa wastaafu kutoka katika mikono ya matapeli nchini.
Hayo yamebainishwa leo Mei 13,2024 mkoani Morogoro na Mhasibu Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Kitengo cha Pensheni, CPA Jenipha Josephat Ntangeki.

Ni katika siku ya kwanza ya Kongamano la Elimu kwa Wamiliki wa Mitandao ya Kijamii nchini ambalo linaendelea hadi Mei 14,2024 katika ukumbi wa Mikutano wa NaneNane mkoani Morogoro.
"Kwa hiyo, Serikali ina mpango wa kutengeneza Wastaafu Portal ili wastaafu hawa, mtu anaweze akapata taarifa zake zote kupitia portal au baadaye mbeleni kutengeneza mfumo utakaomuwezesha mstaafu kujihakiki yeye binafsi pasipo kutembea kwenda ofisi fulani.

"Au pasipo kuhitaji kupigiwa simu na mtu, kwamba kama itafika tarehe tano haujafika, pensheni yako inakata na leo ni tarehe tatu, kwa hiyo ili tukusaidie pensheni yako isikate nitumie shilingi elfu hamsini nitafanya namna, hapana.

"Lengo ni kuondoa huyu mtu wa katikati anayeweza kujikuta anatumika na kujipenyeza kama daraja katikati ya mstaafu na Serikali au katikati ya mstaafu na taasisi zingine zinazotoa huduma za mafao.

"Yote hayo Serikali inalenga kuhakikisha wastaafu wanapata huduma bora pasipo usumbufu wowote,"amesisitiza CPA Ntangeki.
Pia, amesema huduma za mafao ya wastaafu wanaolipwa na Wizara ya Fedha ama HAZINA zinatolewa bure na kuwaasa wastaafu kujiepusha na matapeli wanaowarubuni wawapatie fedha ili wawasaidie kupata mafao yao haraka.

"Kwa hiyo inapotokea mtumishi anakaribia kustaafu ama amestaafu, lakini bado hajapata mafao yake mtu sahihi wa kuwasiliana naye ni yule aliyekuwa mwajiri wake.

"Kwa sababu ndiye ambaye Serikali inamtumia kuwasiliana kwa ajili ya kupata taarifa zake zote zinazohitajika ili aweze kuhudumiwa.

"Lakini, kwa wale wazee ambao tayari walikwisha kustaafu, hawa wazee pia wanayo mahitaji mbalimbali ambayo wanayahitaji kupitia zile taasisi zinazowahudumia.
"Tunao wastaafu wetu, lakini pia tunao wategemezi wa wastaafu, kwa hiyo hao wastaafu na wategemezi wa wastaafu njia sahihi ya kwao wanayotakiwa kuitumia ni kupitia mawasiliano.

"Wizara imetengeneza Call Centre ambayo namba ya mawasiliano ni 0262160000 mstaafu akipiga simu hii, anapiga bure kabisa bila kuchajiwa hata shilingi kumi, na anapata huduma moja kwa moja kutoka kwenye Ofisi za Pensheni.

"Na kupitia namba hii, maana yake ndiyo njia ambayo ni salama kwa wale wazee wetu ambao hawana sanduku la posta au hawana namna ya kuandika barua.

"Kwa sababu tuna namba hiyo, lakini pia kwa njia ya barua, pia wizara inatumia njia hiyo kuwasiliana na hawa wastaafu ambao tayari wanahudumiwa na Wizara ya Fedha, au mtegemezi wa mstaafu aliyekuwa anahudumiwa na wizara.
"Katika kutatua changamoto hii ya matapeli, pamoja na Serikali kuamua kutumia njia sahihi za kuwasiliana na hawa wastaafu au na wale wastaafu watarajiwa wale ambao wanajiandaa kutoka maofisini, bado hawajaingia katika hatua ya kuanza kuchukua mafao yao, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari, maonesho, Wiki ya Utumishi wa Umma na Wiki ya Fedha huko kote elimu inafika.

‘’Kwani Kustaafu ni ghafla? Kustaafu maana yake ni kushindwa kupata kile kipato ambacho umekuwa ukikipata siku zote."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news