NA GODFREY NNKO
MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),Jaji Mshibe Ali Bakari amewapongeza watumishi wa mamlaka hiyo kwa kuendelea kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa na kwa wakati, hatua ambayo imeendelea kuwapa heshima kubwa kwa umma wa Watanzania.
Jaji Bakari ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa mamlaka hiyo, ameyasema hayo Aprili 30, 2024 mkoani Morogoro. Baraza hilo limewakutanisha wajumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Mengi ameyazungumza Mkurugenzi Mkuu, lakini ninataka kuwapongeza. Mnachokisema, mnachokitabiri kwa asilimia 95 kinatokea.
“Mimi kwa uzawa nimetokea Pemba, mnakujua Pemba? Kuna watu matatamatata kule na tunajuana sote, walinipigia hapo mvua ilipochelewachelewa.
“Mwenyekiti vipi? Si tunataniana sana Zanzibar kule, Mwenyekiti mmetudanganya bwana mmesema kutakuwa na mvua…hivi na hivi mpaka leo kukavu.
“Nikawaambia subirini,nikamuuliza Masoud vipi mbona watu wanauliza huko? Wajibu hivyo hivyo wasubirini, wakapigwa na mawingu ya siku saba…
“Wanasema, Mwenyekiti basi nikawaambia mimi siye ni Mwenyenzi Mungu.Kwa ufupi tu, Pemba imenyesha mvua ya ajabu kuliko Unguja, Pemba wamepata mvua nyingi ambayo ni ile ile mliyoisema ndiyo ile ile iliyokwenda, haikupungua.
“Tunawapongeza kwa hilo daktari, watu wanaiamini TMA kwa asilimia 100 na endeleeni kutabiri kama mnavyotabiri na mambo yatakuwa mazuri.”
Vile vile, Jaji Bakari amewakumbusha watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi.
Awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt.Ladislaus Chang’a amesema, madhumuni makuu ya kikao hicho ni kupokea, kujadili na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Amesema, bajeti hiyo ni kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/ 2025. “Bajeti ya TMA inayopendekezwa imeandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele na malengo ya mamlaka kama yaliyoainishwa katika Mpango Mkakati wa Mamlaka wa mwaka 2021/22 na 2026/2027 lakini pia inazingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa na mikakati mingine ya kimaendeleo.”
Amesema, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mchango wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha miundombinu.
“Ninaendelea kushukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo mkubwa.”
Kuhusu TMA
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na.2 ya mwaka 2019 kupitia Tangazo la Serikali GN 459 la Juni 14, 2019.
Ikiwa na jukumu la kuratibu, kudhibiti na kutoa huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
TMA ni zao la iliyokuwa Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania ulionzishwa kwa Sheria ya Wakala (Executive Agency Act) sura Na. 245 marejeo ya mwaka 2022.
Kabla ya Wakala wa Hali ya Hewa, huduma za hali ya hewa nchini zilikuwa zinatolewa na iliyokuwa Idara ya Hali ya Hewa nchini (Directorate of Meteorology) ambayo ilianzishwa mwaka 1977.
Ni baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa na jukumu la kufanya uangazi na kutoa taarifa za hali ya hewa nchini.
Kabla ya Jumuiya ya Afrika Mashariki huduma za hali ya hewa nchini zilitolewa chini ya Taasisi ya Hali ya Hewa iliyokuwa chini ya wakoloni. Aidha, mamlaka inamiliki Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo mkoani Kigoma.
Tags
Baraza la Wafanyakazi TMA
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
TMA Tanzania