DODOMA-Watumishi wa Tume ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) ,makao makuu Dodoma wamepatiwa mafunzo yanayolenga kuongeza ufanisi katka uwajibikaji wa taasisi hiyo.Pia,mafunzo hayo yanalenga kutoa mwongozo kabambe sekta ya umwagiliaji na kuimarisha utendaji kazi kwa watumishi hao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika jijini Dodoma, Mkurugenzi Idara Utawala na Rasilimaliwatu, Maria Itembe amesema, mwongozo huo unasisitiza ushirikishwaji wa wakulima, wilaya, mikoa na ngazi ya kitaifa, katika utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.
Alisema, uwezeshwaji wa watumishi utawawezesha wakulima na kufikia lengo la kuwa wamiliki wa miradi.
“Wakulima hawa wakiwa wamiliki wa miradi wataweza kuitunza na kushiriki kuanzia hatua ya uibuaji wa miradi, utekelezaji wa miradi na uendeshaji na matunzo ya miradi ya umwagiliaji,”amesema Maria.
Aidha, amesisitiza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo waajiriwa wapya wa Tume, ili waweze kuhakikisha uboreshaji wa mchakato wa utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji unafikiwa na wadau wote wanafanya kazi kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yao.
Hata hivyo, alihimiza haja ya uwajibikaji katika kufanikisha mwongozo Kabambe wa Umwagiliaji, ambao utasaidia ukamilishaji wa miradi ya umwagiliaji kwa wakati.
Ametumia fursa hiyo, kuhimiza ufanisi na upatikanaji wa matokeo chanya katika miradi inayotekelezwa na NIRC nchini.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika mkoani Dodoma, yamehusisha watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji makao makuu na baadhi ya watumishi wa tume Mkoa wa Dodoma.