Wauza mlima wa Serikali shilingi milioni 20, DC Shaka acharuka

MOROGORO-Jeshi la Polisi wilayani Kilosa mkoani Morogoro limewatia mbaroni watu wawili akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Msowero A, Petro Sanga (Paroko) na mwenzake, Awadh Ngajime kwa tuhuma za kuuza ardhi (eneo la mlima) mali ya Kijiji cha Msowero wilayani humo.
Jumla ya wananchi 50 wanadaiwa kuhusika katika kuuza Mlima Gongwe wenye ukubwa wa ekari 1,128 kwa watu mbalimbali kutoka nje ya wilaya kwa ajili ya shughuli za kilimo na ujenzi wa makaazi na wengine kuvamia kuweka makazi na kilimo ambapo imebainika kuna uharibifu mkubwa wa mazingira.

Pia, jeshi linaendelea kuwatafuta watu wengine 48 ambao wanaosadikiwa kuwa sehemu ya mtandao uliohusika kuuza kinyume na utaratibu ekari 1,158 za kijiji zilizopo katika mlima huo.

Hayo yamebainika wakati wa mkutano wa hadhara kusikiliza kero za wananchi katika Kata ya Msowero ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa,Shaka Hamdu Shaka mwishoni mwa wiki kijjijini hapo.

Shaka alisema, kumekuwa na wimbi la uvamizi wa maeneo ya ardhi unaoonekana kukithiri siku hadi siku na baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakihusika kuyauza kinyume na sheria.
“Tuna kata saba ndani ya wilaya hii zinaongoza kwa migogoro ya ardhi ikiwemo hii ya Msowero, mnaongoza mnavamia maeneo ya Serikali, viongozi wapo mnashirikiana nao wengine kisha mnageuka mnasingizia viongozi wa wilaya mkoa na taifa kuwa wanakuja kupora ardhi yenu kumbe ni uongo kabisa.

“Mmeuza mlima kinyume na utaratibu ekari 1,158 zote mmevamia na kuuza, hii ni mali ya serikali ya kijiji kisha mnageuka kushutumu wengine kumbe ninyi wenyewe ndio wahusika, OCD huyu mwenyekiti aliyeshiriki kuratibu mauziano na kulipwa 500,000 na huyu aliuza eneo la mlima kwa shilingi 20,000,000 unaondoka nao, pia naagiza watu wengine 48 waliohusika kwenye kuuza wajisalimishe polisi, vinginevyo watafutwe popote walipo na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

Hata hivyo, Shaka alipiga marufuku na kuweka zuio la kuendeleza shughuli yoyote katika eneo la mlima unaodaiwa kuuzwa huku akisisitiza kuwa waliouziwa maeneo hayo wametapeliwa na bado ni mali ya Serikali.

“Viongozi mpo mnayaona kitongoji, kijiji, kata wote mnajua, lakini mnalea uovu huu, haiwezekani kila aliyehusika kwenye hili hatabaki salama ili iwe fundisho kwa wengine, naomba wajuilisheni wote walionunua eneo lile wametapeliwa na hatutasita kuchukua hatua kwa yoyote atakayekaidi maelekezo ya Serikali.

“Kibaya zaidi baada kufanya uovu mnatafuta watetezi ambao na wao kwa kukosa busara na sababu wanatafuta umarufu wa kisiasa, wanalibeba jambo bila kulifanyia utafiti na kujridhisha kumbe mnawaingiza mkenge.
“Nilishangaa sana viongozi wa chama kimoja cha siasa wakilibeba jambo hili wakidai wananchi wananyang'anywa ardhi wanapigwa na kuindoshwa katika maeneo yao, kumbe mumewalisha matango pori mnaficha uovu wenu na wao kwa vile maarifa yao madogo wakaona ndio ajenda ya kuibeba limebuma, sasa warudi kukanusha uongo waliouaninisha umma wa watanzania,"alifafanua Shaka.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msowero,Abdalla Machera alimueleza mkuu wa wilaya kuwa, katika siku za karibuni viongpzi wa kisiasa wamekuwa wakifika katika maeneo yao huku wakilazimisha wananchi kupigwa picha na kutoa malalamiko ama shutuma za uongo dhidi ya serikali jambo ambalo amesema sio la kiungwana na kistaarabu.

"Mheshimiwa DC unayoyasikia huko ni kutaka kuchafua kata yetu na viongozi wetu ninyi ili wao kutafuta kuungwa mkono kwa mambo ya uongo na uzushi, yaliopo hapa ni baadhi ya wananchi kujihusisha katika matendo maovu sasa wakiona mnataka kuwachukulia hatua wanakimbilia kwa viongozi wa kisiasa ili wapaze sauti wakidhania wanaweza kuzima uovu wao wasichukuliwe hatua kwa makosa yao, haiwezekani, wameuza mlima wetu ekari 1158, ″alisema Abdallah Mkweche Mwenyekiti wa Kijiji cha Msowero.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news