Wazee Arusha waipongeza DCEA udhibiti dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO 

WAZEE kutoka kata 25 za Jiji la Arusha wameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kuonesha umahiri mkubwa katika udhibiti wa dawa hizo hususani bangi mkoani Arusha.
Pongezi hizo wamezitoa mwishoni mwa wiki baada ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha kutoa semina maalum juu ya madhara ya tatizo la dawa za kulevya na rushwa.

Semina hiyo ya dawa za kulevya na rushwa ilitolewa kwa wazee 35 kutoka kata 25 za Jiji la Arusha.

Mgeni rasmi wa semina hiyo hiyo maalum alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mheshimiwa Felician Mtahengerwa.
Kwa niaba ya wazee wenzake, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Kata ya Moshono jijini Arusha, Mzee Ndoomana amebainisha kuwa, DCEA chini ya Kamishna Jenerali Aretas Lyimo imekuwa ikifanya kazi kubwa na matokeo yanaonekana.

"Jitihada zinazofanyika juu ya kuondoa tatizo la bangi katika mkoa huu wa Arusha, ninataka kuipongeza ile taasisi hasa yule Jenerali Lyimo.

"Nilikuwepo kwenye ule uzinduzi uliofanyika hapa Arusha, alionesha umahiri mkubwa hasa katika yale maeneo yanayolima bangi,kwa maeneo makubwa na kwa ustadi mkubwa ambapo kile kinachoitwa cha Arusha ilikuwa inafahamika ndiyo bangi kali.
"Sasa nataka nimpongeze na baraza hili la wazee limpongeze sana yule Mheshimiwa (Kamishna Jenerali Aretas Lyimo) kwa sababu Arusha inaingiza watalii wengi kutoka duniani, kwa kupunguza bangi peke yake itatoa sifa kubwa katika mkoa huu wa Arusha hasa jiji hili la Arusha.

"Nilikuwa naomba taasisi hii itufikie katika maeneo yetu ya kata, tunakofanya mikutano ya wazee au aidha mikutano ya jumla ya kata ili waweze kusambaza taaluma (elimu) hii na itasaidia sana kupunguza, sisi kama wazee tusiwe na huruma nyingi maana huruma ikizidi huwa inazaa dhambi.
"Tumekuwa na kama kusaidia au ulezi mbovu bila vijana wetu kuwakemea, kijana akikamatwa akipelekwa polisi,Mzee unaenda kutoa rushwa ili kijana atolewe kwa ajili ya bangi.

"Muache aende kule polisi, kule Magereza anaenda kukutana na kina Lazaro na akina nani...mwisho akirudi hapa atakuwa mtu mwema,lakini mkiwa na huruma nyingi, na imekuwa ni shida,"amesisitiza Mzee Ndoomana.
Pia, amewataka wazee hao kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na vyombo vingine vya usalama kuwafichua vijana na watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya mkoani humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news