Waziri Dkt.Nchemba awapa habari njema wafanyabiashara nchini

DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewahakikishia wafanyabiashara nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi hususani wafanyabiashara katika maendeleo ya nchi na kuahidi kuwa itaendelea kuzifanyiakazi changamoto zinazokwaza ustawi na mazingira ya ufanyaji biashara hususani ya kikodi.

Dkt. Nchemba alitoa ahadi hiyo jijini Dar es Salaam wakati Viongozi wa Wizara za kisekta wakiongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), walipokutana na Viongozi wa Kitaifa na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili masuala mbalimbali kwa jili ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara katika Soko hilo la Kimataifa.
Dkt. Nchemba, aliwaasa wafanyabiashara hao kuachana na mambo ya kuitisha migomo wanapotaka kuwasilisha hoja ama malalamiko yao badala yake watumie fursa na nia njema ya Serikali ya kuwasikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili kwa njia ya mazungumzo.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuwa waaminifu na kulipakodi za Serikali kwa hiari ili fedha zinazopatikana zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Tume ya Ushindani, Jijini Dar es Salaam, uliwashirikisha Viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Viwanda na biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Daniel Sillo (Mb), Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, Naibu Katibu Mkuu-Tamisemi (Miundombinu), Mhandisi Rogatus Mativila, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya na viongozi wengine waandamizi wa Serikali pamoja na wawakilishi wa Wafanyabiashara nchini pamoja na Soko Kuu la Kariakoo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news