Waziri Mchengerwa akasirika

MOROGORO-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, atavunja mabaraza ya madiwani yenye mivutano inayokwamisha maendeleo ya wananchi.
Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo wakati wa kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya inayojengwa Kata ya Kibelege katika Halmashauri ya Mji Ifakara mkoano Morogoro na kubaini kuwa imeshindwa kukamilika kutokana na mivutano ya kisiasa uliotokea mara tu fedha za ujenzi wa hospitali hiyo zilipofika.

Amesema, mivutano ya kisiasa ya madiwani husababisha miradi mbalimbali ya maendeleo kusimama na kutokamilika kwa wakati na kusisitiza kuwa atachukua hatua mara moja ikiwa ni pamoja na kuvunja Baraza la Madiwani la halmashauri husika.
Aidha, Mchengerwa ametumia fursa hiyo kuwaagiza watendaji katika halmashauri nchi nzima kuacha mivutano na wanasiasa na kusababisha ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo.

Amesisitiza kuwa, pia itampasa kuwachukulia hatua watendaji hao waliohusika ikiwa ni pamoja na kuwashusha madaraka yao.

"Mnapovutana wanasiasa na watendaji, watendaji wanashindwa kufanya maamuzi, mkifanya hivyo mjue mnawanyima haki wananchi kupata huduma, sasa sitaki kusikia mivutano kwenye mabaraza ya madiwani.

"Popote nitakaposikia kuna mivutano kama Waziri mwenye dhamana nitavunja Mabaraza ya Madiwani kwa maslahi mapana ya wananchi," amesema.

Waziri Mchengerwa ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wakurugezi wa halmashauri zote nchini kushungulikia migogoro inayoibuka kwenye halmashauri zao na kama wameshindwa kuimaliza anapaswa kutoa taarifa haraka katika Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
"Kunapoibuka migogoro na mivutano wakurugenzi mnapaswa kuishughulikia haraka na mkishindwa basi ripoti Ofisi ya Rais-TAMISEMI na sio kukaa kimya na kuendelea kuchelewesha maendeleo kwa wananchi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news