Waziri Mchengerwa ashuhudia athari za maafa ya mvua, aagiza TARURA ipewe fungu la dharura daraja la Mbuga Ulanga

ULANGA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu kuipatia TARURA kiasi cha shilingi milioni 250 za dharura kwa ajili ya kujenga daraja la muda la Mbuga katika mto Luhombero.
Sambamba na ukarabati wa daraja la waenda kwa miguu la Chigandugandu wilayani Ulanga yaliyoharibiwa kutokana na mafuriko.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwaya na Mbuga ambao kwa sasa hawana mawasiliano na inawalazimu kutumia mtumbwi wa kuvutwa kwa kamba,Waziri Mchengerwa amesema, kwa adha wanayopata wananchi hao daraja la muda haliepukiki mahali hapo.

“Ndugu zangu kwanza tupate daraja la muda litakalowawezesha wananchi kupita wao wenyewe pia kupitisha mazao yao katika msimu huu wa mavuno,hatuwezi kutimiza malengo yetu kama daraja hili bovu."
Waziri Mchengerwa amesema,kwa siku tatu za ziara yake kwenye wilaya zilizopata mafuriko mkoani Morogoro ameshuhudia maeneo mengi yaliyopata uharibifu mkubwa wa miundombinu na kumuagiza Katibu Mkuu kuipatia TARURA shilingi milioni 250.

Hata hivyo, alitoa maelekezo kwa TARURA kuanza mara moja mchakato wa dharura wa ujenzi wa daraja hilo na kuwapa mwezi mmoja na nusu kulikamilisha.

Aidha, Waziri Mchengerwa aliwasıhi wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo kwani Rais anaendelea kuwajali wananchi wake na kuiangalia Ulanga hususani kwenye miundombinu.
“Fedha tunazoleta hapa ni fedha za wananchi ambazo tunaelekezwa na Mhe. Rais,msingi wa serikali ni wananchi.”

Aliongeza kwamba,Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwajali wanyonge pamoja na wananchi wa Mbuga na Mwaya, hivyo fedha za dharura zinazotemgwa zinaenda kutibu na kuimarisha uchumi wa wananchi.

“Rais anawajali wanyonge na wananchi wake ndio maana akatoa fedha hizi kwa ajili kwa wananchi wake hususani maeneo ya uzalishaji na kimkakati ili wananchi waendelee kupata huduma pia wakulima wa mazao ya chakula na biashara waweze kuendelea na shughuli zao.”
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Mhe. Adam Malima amesema, daraja hilo ni la kiuchumi,pia maisha ya watu yanahitaji daraja hilo, kwani wakulima walikuwa wanatumia mtumbwi kuvusha mazao yao.

Amesema, ni vyema kuanza kujenga vivuko vya muda katika mkoa wake ili kuweza kuwavusha wananchi na mali zao wakati wanasubiri kujengewa daraja la kudumu.

Awali Mbunge wa Ulanga, Mhe. Salim Hasham amesema, Kata ya Mbuga ina watu wengi na ndio inayoongoza kwa uzalishaji wa zao la pamba na ufuta ambapo inaifanya Mahenge kuwa na zao la biashara.

Amesema,matatizo ya Ulanga ni makubwa ila tatizo la daraja hilo ni kubwa zaidi na amemshukuru Waziri kufika eneo hilo ambalo wananchi wa Kata ya Mwaya na Mbuga walikuwa wakipata adha ya usafiri hususani wagonjwa.
Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Mbuga, Mhe. Said Mfaume amesema, daraja hilo litakuwa mwarobaini wa kuwasaidia wananchi wa kata yake, kwani kata hiyo inazalisha kwa asilimia 75 ya mazao ya biashara na chakula pia wakazi hao hupata huduma za afya upande wa pili wa Kata ya Mwaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news