DODOMA-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, ameonesha kufurahishwa na Mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanayotolewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa watu wenye ulemavu.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa, amekitaka Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania kufanya jitihada za kujitanua katika mafunzo hayo ya TEHAMA kwa walemavu ili kuwafikia hata waliopo katika sehemu mbalimbali za nchi ili kutanua wigo wa matumizi ya TEHAMA kwa makundi hayo ya walemavu.
Akiongea katika maonesho hayo Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Uongozi na Menejimenti katika Teknolojia ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Catherine Mkude, amemshukuru Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Nape Nnauye, kwa kutoa mwaliko kwa chuo hiki kushiriki maonesho haya.
Dkt. Mkude, ameongeza kuwa maonesho haya yamekuza wigo wa ufahamu wa elimu ya TEHAMA kwa walemavu kwa viongozi na wabunge ambao watakwenda kuwafahamisha wananchi katika majimbo yao.

