MBEYA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya za Kyela na Rungwe zilizoko mkoani Mbeya waangalie namna ya kufanya uwekezaji mkubwa kwenye fukwe za Matema (Matema Beach) ili kukuza utalii wa eneo hilo.
“Nimeenda Matema Beach, nimeona jinsi fukwe za Ziwa Nyasa zilivyo nzuri. Nendeni mkawekeze kwenye zile fukwe ili kuongeza kivutio cha utalii lakini pia mtawezesha watu wa wilaya za jirani zikiwemo hizi mbili waweze kwenda kupumzika wikiendi,” alisema.
Alitoa wito huo jana jioni Jumapili, Mei 12, 2024 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa wilaya za Kyela na Rungwe ambako alikuwa na ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.
Aliwaeleza wananchi hao hatua ambazo zimefikiwa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali kwenye sekta za elimu, afya, maji na miundombinu na kuwataka waendelee kuwa na imani na Serikali yao kwa sababu ina dhamira ya dhati ya kuendelea kuwatumikia.
Alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Renatua Mchau afuatilie maagizo ya Serikali yaliyolenga kuhakikisha kuwa maeneo ya shule za msingi na sekondari yanawekewa alama na uzio ili kuzuia uvamizi wa maeneo hayo.
“Tulishatoa maelekezo kuwa maeneo yote ya taasisi kama hizo yapimwe na kuwekwa uzio. Mkurugenzi uone tuna shule ngapi hapa na zipi ziko kwenye hatari ya kuvamiwa. Wekeni alama na kujenga uzio, siyo lazima uwe wa matofali, mnaweka kuweka fensi ya waya,”alisema.
Mapema, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu alisema ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa Tukuyu ambayo ni makao makuu ya wilaya umefikia hatua za mwisho na uko kwenye majaribio ili kubaini kama kuna mapungufu yoyote.
“Hapa Tukuyu, tuna mradi wa shilingi bilioni 4.5 ambao umekaribia kukamilika na mkandarasi yuko anajaza maji kwenye tenki ili aweze kufanya majaribio na kubaini kama kuna mapungufu yoyote kabla mradi huo haujaanza kutumika,” alisema.