NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema, Serikali imefanikiwa kusajili wanafunzi 22,131 wakiwemo wasichana 2,794 wa elimu ya sekondari kwa njia mbadala.
Ni katika vituo vya elimu ya watu wazima pamoja na kutoa mafunzo ya kisomo kuimarisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa watu wazima 6,238 katika mikoa 26 nchini.
Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo Mei 7,2024 wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma.
Pia, amesema kuwa Serikali imekamilisha moduli 11 za hatua ya I na ll kwa ajili ya vituo 151 vya elimu ya sekondari kwa njia mbadala ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika vituo hivyo.
Vile vile, Mheshimiwa Waziri Mkenda amesema, Serikali imeongeza idadi ya vituo vya elimu ya sekondari kwa njia mbadala kutoka 168 hadi kufikia 190 kwa lengo la kuongeza fursa kwa wanafunzi waliokosa elimu kwa sababu mbalimbali nchini.
Mbali na hayo, Prof.Mkenda amesema,Serikali imeendelea kuimarisha fursa za upatikanaji wa elimu ya juu kupitia utoaji wa mikopo kwa wanafunzi.
Amesema, Serikali pia imetoa ufadhili kwa wanafunzi 1,220 kati ya 1,200 waliolengwa ambapo wanafunzi wapya ni 915 na wanaoendelea ni 305 wenye jumla ya Shilingi bilioni 6.4 kupitia Samia Scholarship.
“Serikali pia imetoa mikopo kwa wanafunzi 2,299 wa ngazi ya stashahada yenye jumla ya shilingi 6,114,790,500.00 na imekusanya jumla ya shilingi 132,731,358,063.47 sawa na asilima 55 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 241 kutokana na mikopo iliyoiva.”
Wakati huo huo, Prof.Mkenda amesema,Serikali imeendelea kuimarisha udhibiti na kukuza matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.
Amesema, Serikali imesajili vituo vipya 43 vya Mionzi ayonishi na kufikisha jumla ya vituo vya mionzi 1,386 vilivyosajiliwa na vituo vipya 42 vya mionzi isiyoayonishi na kufikisha jumla ya vituo vya mionzi isiyoayonishi 409 vilivyosajiliwa.
Waziri Mkenda amesema, Serikali imesajili vyanzo vipya 36 vya mionzi na kufikia jumla ya vyanzo vya mionzi 1,647 vilivyosajiliwa.
"Serikali imetoa leseni 633 za kumiliki na kutumia vyanzo vya mionzi, uingizaji nchini wa vyanzo vya mionzi 95, utoaji nje ya nchi wa vyanzo vya mionzi 13 na safirishaji wa vyanzo vya mionzi ndani ya nchi 47; imepima viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 1,980 wanaofanya kazi katika vyanzo vya mionzi katika vituo 429.
"Aidha, viwango vya mfiduo vilivyopokelewa katika miezi mitatu mfululizo vilianzia 0.1 hadi 3.2 millisievert (mSv), ambavyo viko ndani ya ukomo unaokubalika wa udhibiti."
Mwaka ujao
Katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 Waziri Mkenda amesema, wizara yake inataria kutumia zaidi ya shilingi trilioni 1.96 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele vitano.
Lengo ni kuhakikisha ubora wa elimu nchini unazidi kuimarika hivyo kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajiriwa kupitia ujuzi maarifa.
Pia, amesema Serikali itafanya mapitio ya mitaala 171, kuandaa mitaala mipya 18, kuanzisha programu za vipaumbele 145.
Sambamba na matumizi ya mbinu bunifu za ufundishaji katika elimu ya juu ili kuwawezesha vijana kuwa na ujuzi zaidi.
Waziri Prof.Mkenda amesema, pia Serikali itawezesha ujenzi wa shule mpya 100 za sekondari za ufundi, kati ya hizo shule 26 zitaanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari mwaka kesho.
Amesema, ujenzi wa shule za amali utapewa kipaumbele katika maeneo ambayo hayana vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi au shule ya amali ya sekondari.
Vile vile, amesema wataendelea na ujenzi wa karakana nne kwa ajili ya fani ya umeme, ufundi bomba, ufundi magari na ujenzi katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo Stadi kilichopo Kihonda.
Sambamba na ujenzi wa karakana ya ufundi bomba katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo Stadi cha Mkoa wa Mbeya.
Pia, amesema Serikali itadahili wanafunzi 263,718 wa elimu ya ufundi na mafunzo na ufundi stadi ambapo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi ni 190,518 na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ni 73,200 sawa na ongezeko la asilimia 23 ikilinganishwa na udahili wa mwaka 2023/24.
Prof.Mkenda amesema,udahili unalenga kuongeza rasilimaliwatu yenye ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kwa wanafunzi hao.
Kuhusu mikopo, Prof.Mkenda amesema,Serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada takribani 10,000 katika fani za kipaumbele na zenye uhaba wa wataalam nchini ikiwemo fani za sayansi na ufundi.
Amesema, ili kuwezesha na kuimarisha huduma ya utoaji na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa na uhitaji, Serikali itaongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka 223,201 hadi 252,245.
Waziri amesema, Serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi 84,500 wa mwaka wa kwanza ambapo shahada ya kwanza ni 80,000, shahada za juu 2,000, wanaosoma nje ya nchi 500 na Samia Scholarship ni 2,000
Vile vile watatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 40 wenye ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi hususani wanafunzi wa kike waliohitimu Mtihani wa Taifa ya Kidato cha Sita na shahada ya awali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Vipaumbele vitano 2024/25
Waziri Prof.Mkenda ametaja vipaumbele vya Wizara Elimu kwa mwaka wa fedha 2024/25 kuwa ni pamoja na;
i:Kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini
ii:Kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (amali na amali sanifu);
iii:Kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu;
iv:Kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu; na kuendeleza tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
V:Kuendelea na utekelezaji wa Sera na Mitaala, Mapitio ya Sheria na kuandaa Miongozo ya Utoaji Elimu na Mafunzo Nchini“