Waziri Silaa afunga Ofisi ya Masijala ya Ardhi jijini Dodoma

MUNIR SHEMWETA
NA ELEUTERI MANGI

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa amefunga Masijala ya Ardhi ya Jiji la Dodoma ikiwa ni hatua ya wizara yake kuondoa changamoto za sekta ya ardhi katika jiji hilo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhe. Jerry Silaa (kulia) akifunga kofuli kwenye Ofisi ya Masijala ya Ardhi ya jiji la Dodoma alipokwenda kuzifunga rasmi ofisi hizo leo Mei 28, 2024.

‘’Tumeamua kufunga masijala hii ya jiji, nimetoka kuweka makufuli tumeifunga. Tunahamisha shughuli hizi za ardhi kutoka hapa kuja ofisini kwangu kwa Waziri wa Ardhi.

"Na shughuli hizi tumezitoa hapa kwa sababu huyu aliyenyoosha mkono wa mwaka 2017 nikimpa nafasi aelezee mimi nakosa majibu kama waziri mwenye dhamana ya ardhi," amesema Mhe.Jerry Silaa.

Akizungumza na wananchi baada ya kufunga kofuli kwenye masijala ya ofisi ya ardhi jiji la Dodoma leo Mei 28, 2024 Mhe.Silaa amemuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kusimamia shughuli hiyo ili kuhakikisha watu wanapata haki zao.

‘’Dkt.Samia ametuelekeza tusimamie haki za watu wake, na kazi hiyo tutaifanya kwa uadilifu mkubwa na ukisoma vitabu vyote vya vinaelezea kazi ya haki ni kazi ya Kimungu,’’ amesema Mhe. Silaa.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhe. Jerry Silaa (kulia) akimkabidhi funguo Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga mara baada ya kuzifunga ofisi ya Masijala ya Ardhi ya jiji la Dodoma leo.

Amewaambia wananchi waliokwenda kupata huduma wakati wa kufunga ofisi hizo za masijala ya ardhi ya jiji la Dodoma kuwa, ofisi za ardhi sasa zitafunguliwa rasmi siku ya Jumatatu ya Juni 3, 2024 kweye ofisi za ardhi iliopokuwa ofisi za Halmashauri ya jiji la Dodoma zamani.

Aidha, amesema, wizara yake itajenga ofisi ya kisasa yenye kamera zenye uwezo wa kuchukua sauti itakayosimamiwa moja kwa moja na ofisi ya waziri pamoja na Katibu Mkuu sambamba na kuweka maafisa waadilifu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhe. Jerry Silaa (katikati) akizungumza na wananchi mara baada kufunga ofisi ya Masijala ya Ardhi ya jiji la Dodoma leo. Kushoto ni Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga na kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Lucy Kabyemera.

‘’Naenda kujenga ofisi ya kisasa itakuwa na jicho langu mimi moja kwa moja tutaweka maafisa waadilifu, binadamu wa siku hizi siyo binadamu wa zamani tutaweka kamera zitachukua picha na sauti na wakati nikiwa Dar es Salaam na jimboni katika ziara nina uwezo wa kuingia kwenye simu yangu kuangalia ofisi za ardhi Dodoma wanafanya nini,’’amesema Mhe. Silaa.

Kwa mujibu wa Waziri Silaa, muelekeo wa Wizara ya Ardhi ni kujenga ofisi za kisasa ambazo wananchi watakuwa wakipata huduma kwa wakati mmoja usiokuwa na vyumba vya kujifungia.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhe. Jerry Silaa akizungumza na wananchi baada kufunga ofisi ya Masijala ya Ardhi ya jiji la Dodoma leo. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Awali akiongea na watumishi wa ardhi ofisi ya jiji la Dodoma katika ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma, Mhe. Silaa amewataka watumishi hao kuwajibika wakati wa kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kila siku ya kuwahudumia wananchi kwenye sekta ya ardhi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhe. Geophrey Pinda amewataka watumishi hao wa sekta ya ardhi kuwa tayari na kupokea mabadiliko yenye utendaji kazi wenye tija yatakayoleta uhai katika maisha ya watu.

‘’Daima lazima akili yako ihisi kwamba badiliko lolote kwako ni darasa,’’amesema Mhe. Pinda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news