Waziri Simbachawene awataka wahitimu wa mafunzo ya uongozi kuwa mfano bora kwa jamii

DAR-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amewataka Wahitimu wa Mafunzo ya Uongozi kuwa mfano katika jamii na kutumia taaluma waliyoipata kwa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, uwazi na haki.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo Mei 17,2024 katika Ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya saba ya wahitimu wa mafunzo ya uongozi yanayotolewa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Chuo cha Aalto EE cha Nchini Finland.
“Mafunzo ya uongozi yanathamani kubwa sana, hivyo, tunataka kuona uongozi wa kimkakati wenye manufaa zaidi katika usimamizi wa rasilimaliwatu na fedha, tunataka kuona mnaboresha nyanja ya mawasiliano na mahusiano baina yenu na wadau wengine wa masuala ya maendeleo ndani na nje ya nchi,” amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa Kiongozi mzuri ni yule anayewajibika na kuhakikisha anaacha alama, kwa mantiki hiyo hategemei kuona wahitimu hao wanakwenda kufanya kazi kwa mazoea bali watatumia uwezo wao na elimu waliyoipata kuleta matokeo chanya kwa ustawi kwa jamii.Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Kikwete amewataka wahitimu hao kuwa chachu na kuleta mapinduzi katika maeneo yao ya kazi huku akiwasisitiza kuendelea kusoma zaidi kwa manufaa yao na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Kutokana na taarifa ya mafunzo mliyopata, mimi binafsi sitarajii kusikia wala kuona mnaendekeza tabia ya kutumia simu muda wa kazi wakati wananchi wanasubiri huduma na majibu ya changamoto zinazowakabili,” alisema Mhe. Kikwete.

Aidha, Mhe. Kikwete ameto rai kwa wahitimu hao kutambua kuwa dhima kubwa ya uongozi ni kuonesha njia sahihi kwa ili kuleta maendeleo ya haraka na yenye ufanisi.Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo amesema, Taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kuandaa na kuendesha mafunzo kwa viongozi, kuendesha majadiliano ya kisera na kufanya tafiti za kisera, kutoa ushauri wa kitalaam na kuzisaidia taasisi mbalimbali pamoja na viongozi wake katika kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news