Waziri wa Fedha atoa rai kwa wadau wa maendeleo nchini

DODOMA-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ametoa rai kwa wadau wa maendeleo nchini likiwemo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kuiunga mkono Serikali katika uelekeo wake wa kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji ili kuondoa umaskini kwa wananchi.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akitoa akitoa rai kwa wadau wamaendeleo kujielekeza kwenye sekta za uzalishaji, wakati wa mkutano na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Shigeki Komatsubara, (hayumo pichani), ambao ulijadili ushirikiano kati ya Serikali na Shirika hilo, jijini Dodoma. Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha Bw. Robert Mtengule na kulia ni Kamishna wa Idara ya Madeni, Bw. Japhet Justine.

Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara ambapo walijadili kuhusu ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Serikali na Shirika hilo.

Dkt. Nchemba alisema kuwa taasisi za Kiserikali na zisizo za kiserikali ziunganishe nguvu ili kuwawezesha wananchi katika maeneo ya uzalishaji na sio semina kwa kuwa kuwekeza kwenye semina hakumuondoi mwananchi kwenye umasikini.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiagana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara, baada ya mazungumzo yao yaliyolenga kuimarisha ushirikiano yaliyofanyika, jijini Dodoma.

“Tuliishafanya sana semina, kuongeza uwezo, huu si muda tena wa mbia anasema anakuja kusaidia halafu anasaidia kwenye semina, tuliisha jifunza vya kutosha, tujielekeze kwenye shughuli za uzalishaji, aje mdau aseme Serikali imejenga Skimu kubwa ya umwagiliaji, mimi najenga hii ya mbogamboga kwa ajili ya wanawake wazalishe mwaka mzima”, alisema Dkt. Nchemba.

Alitoa rai kwa Shirika la UNDP kusaidia kupeleka ujumbe huo kwa wadau wengine, katika kipindi ambacho Serikali imeweka uelekeo kwenye sekta za uzalishaji basi na wadau wengine wote wa maendeleo nchini wachukue mwelekeo huo ili kuweza kuunganisha nguvu katika maeneo hayo ya uzalishaji.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Shigeki Komatsubara, akiipongeza Serikali kwa jitihada zake za kukuza uchumi na kuondoa umasikini wakati wa Mkutano na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayumo pichani), uliojadili namna ya kuboresha ushirikiano, mkutano huo ulifanyika Wizara ya Fedha, Treasury Square jijini Dodoma.
Ujumbe wa Wizara ya Fedha ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) ukisikiliza maelezo ya Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Shigeki Komatsubara, kuhusu kuwekeza kwa ajili ya maendeleo ya baadae, wakati wa mkutano uliojadili ushirikiano kati ya Serikali na Shirika hilo, uliofanyika Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Aidha alisema kuwa katika mazungumzo yao wamejadili maeneo ambayo wanaweza kushirikiana ikiwa ni pamoja na usaidizi wa kitaalamu katika maeneo ya kuongeza uwekezaji ambayo yanaenda sambamba na ajenda kuu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza uwekezaji unaolenga kuongeza ajira kwa watanzania hasa vijana, ushirikiano katika Dira Mpya ya Maendeleo inayoandaliwa na dhana pana ya Uchumi jumuishi usiomuacha mtu yeyote nyuma.

Vilevile alisema kuwa imani yake ni kuona ushirikiano wa kimaendeleo utaendelea chini ya Awamu mpya ya Mfumo wa Ushirikiano Endelevu wa Umoja wa Mataifa (UNSDCF) wa mwaka 2022 hadi 2027, ambao unahusisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Mashirika yaliyo chini yake na Serikali ya Tanzania.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara alisema kuwa anafurahishwa na Tanzania kwa kuwa inasonga mbele kutoka uchumi wa chini na kuwa uchumi wa kati.
Ujumbe wa Wizara ya Fedha ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) ukiwa katika Mkutano na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Shigeki Komatsubara, (hayupo pichani) ambao ulijadili ushirikiano kati ya Serikali na Shirika hilo, uliofanyika Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo zinampa ujasiri kusema ni rahisi uchumi wake kukua kwa kuwa unajengwa kwenye amani, umoja na mshikamano, ambapo jumuiya za kimataifa zinathamini hali hiyo na pia zinamatarajio makubwa kuwa Tanzania itaendelea kuzalisha taarifa nzuri kwa Afrika na Dunia kwa ujumla na kujenga Uchumi jumuishi.

Aidha, alisema kuwa uwekezaji kwa ajili ya baadae utaiwezesha Tanzania kusonga mbele na pia amekaribisha majadiliano kati ya Serikali na Shirika hilo yatakayowezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo kwenye sekta za uzalishaji.
Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje. Bw. Robert Mtengule, akiteta jambo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Shigeki Komatsubara (kulia), baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya Mwakilishi huyo na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (hayumo pichani), yaliyohusu ushirikiano kati ya Serikali na Shirika hilo, yaliyofanyika, jijini Dodoma. Kushoto ni Kamishna Idara ya Madeni, Bw. Japhet Justine.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB) (wa sita kulia) na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Shigeki Komatsubara (wa sita kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania pamoja na UNDP, baada ya mazungumzo yao yaliyolenga kuboresha ushirikiano, yaliyofanyika Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha).

Bw. Komatsubara ameishukuru Tanzania kwa kumpa nafasi kufanya kazi kwa Watanzania na Serikali yake na ameahidi kuongeza ushirikiano kati ya Shirika lake na Serikali na pia kuwa balozi mzuri wa Tanzania katika Shirika hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news