Wizara ya Fedha yatoa rai kwa wadau wa habari nchini

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha imesema, wadau wa sekta ya habari ni nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya uchumi nchini.
Hayo yamesemwa leo Mei 14,2024 na Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Salome Kingdom katika siku ya pili ya Kongamano la Wamiliki wa Mitandao ya Kijamii nchini ambalo limeratibiwa na wizara hiyo mkoani Morogoro.

"Wadau katika sekta ya habari wapo katika nafasi kubwa katika kuchochea maendeleo ya uchumi wetu kwa njia ya kuwahamasisha wananchi kutekeleza kwa pamoja malengo ya Taifa.
"Kwa sababu, wadau kutoka sekta ya habari wataandika na kutangaza taarifa za mipango ya maendeleo, utekelezaji wa mipango ya maendeleo na mrejesho kutoka kwa wanachi juu ya mapokeo ya mipango ya maendeleo,"amesisitiza Bi.Kingdom.

Pia, amesema ni vema wadau wa sekta ya habari kuendelea kushirikiana na sekta ya umma katika kuleta maendeleo nchini.

Mbali na hayo, Mchumi Mkuu huyo ametaja vipaumbele vitano katika utekelezaji wa bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema, miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma.

Vile vile kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu,kuendeleza rasilimali watu na kuchochea uchumi shindani na shirikishi nchini.

Bi.Kingdom amesema, ili kuweza kufanikisha vipaumbele hivyo,Serikali inajielekeza zaidi katika kuongeza mikakati ya ukusanyaji wa mapato ambayo yatatumika kugharamia miradi ya maendeleo nchini.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na hamasa ya kuwahimiza wananchi kila wanapofanya manunuzi ya bidhaa kuhakikisha wanadai risti halali za kieletroniki kulingana na kiasi alicholipia.

Amesema, ili kufikia malengo hayo, vyombo vya habari vinategemewa kuwa daraja muhimu kati ya Serikali na wananchi ili waweze kushiki kikamilifu kulipa kodi ambazo zitawezesha Serikali kufikia malengo.

Amesema, kupitia vyombo vya habari wananchi wanahitaji kusikia mambo gani yamefanyika kupitia kodi zao.
Bi.Kingdom amesema, katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali inakusudia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi trilioni 49.3 ambapo asilimia 70 ya bajeti ikitegemea mapato ya ndani huku asilimia 30 ikitegemea mapato ya nje.

Amesema, kutokana na asilimia 70 ya bajeti kutegemea mapato ya ndani nchini, kila mwananchi ana nafasi kubwa kufanikisha upatikanaji wa mapato hayo.
Bi.Kingdom amesema, mapato ya ndani ni yale yatokanayo na makusanyo ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),malipo mengine yatokanayo na huduma za serikali, mapato yasiyo ya kodi ambayo yanatoka serikali za mitaa na mshirika ya umma, ushuru, faini, gawio na mengineyo.

Mchumi Mkuu amesema,mapato ya nje ni yale yanayotokana na mikopo nafuu na mikopo ya kibiashara ikiwemo misaada ya washirika wa maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news