DAR-Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa Wizara ya Madini itaendeleza juhudi zake katika kuhakikisha inapatia ufumbuzi changamoto zinazokwamisha uendelezaji wa miradi ya madini kwa nia ya kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwa miradi hiyo sambamba na kuchochea maendeleo ya sekta na taifa kwa ujumla.Dkt. Kiruswa amesema hayo Mei 09, 2023 na wakati akimwakilisha Waziri wa Madini katika Mkutano baina ya uongozi wa juu wa Wizara ya Madini pamoja na wanachama wa Chemba ya Migodi Tanzania (Tanzania Chamber of Mines) uliopewa jina la Mining Breakfast Briefing (MBB) uliofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, ili sekta ya madini ilete manufaa chanya kwa upande wa Serikali pamoja na makampuni ya uchimbaji ni vyema kuwepo na ushirikiano wa dhati kutoka pande zote serikali na sekta binafsi ili wananchi waone faida ya uwepo wa rasilimali madini inayopatikana kwa wingi hapa nchini.
Dkt. Kiruswa amesema kwamba, Wizara ya Madini imewezesha kufanikisha mazungumzo kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni zenye miradi ya madini kwa lengo la kupeleka umeme katika miradi hiyo kwa lengo la kutatua changamoto ya nishati ambayo imekuwa ikikwamisha miradi mingi.
Katika hatua nyingine, Dkt Kiruswa amesema kuwa mafanikio makubwa yaliyopo katika Sekta ya Madini hivi sasa yametokana na Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jambo linalosaidia mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa kwa kusaidia kuanzishwa kwa miradi hiyo miradi hiyo.
Katika kulithibitisha hilo, Dkt. Kiruswa ametoa mfano wa kukabidhiwa kwa leseni ya uchimbaji mkubwa (SML) kwa kampuni ya Nyati mineral Sands na pia, leseni ya usafishaji wa madini kwa kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma tarehe 21 Machi, 2024 jijini Dodoma.
Mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa kitakwimu umeongezeka kutoka asilimia 6.7 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 9.1 mwaka 2023.
Dkt. Kiruswa ameongeza kuwa, Wizara ya Madini inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Visioni 2030: Madini ni Maisha na Utajiri ambapo lengo kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia ili kutoka asilimia 16 zilifonyika hivi sasa na kufika asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 na kusisitiza kuwa kufikia lengo hilo, ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi husasan makapuni ya utafiti na uchimbaji wa madini yaliyopo nchini ni muhimu.
Kwa upande Katibu Mtendaji wa Chemba ya Migodi Tanzania (TCM), Mhandisi Benjamin Mchwampaka amesema, kwa hivi sasa, migodi mingi imebadili aina ya uchimbaji kutoka ule wa migodi ya wazi juu ya ardhi na kuwa migodi ya chini ya ardhi (Underground mines), hali ambayo imesababisha uhitaji mkubwa wa mafundi mchundo wenye ujuzi wa kuendesha mitambo mikubwa ya uchimbaji chini ya ardhi na pia matengenezo ya mitambo hiyo.
Ili kuondokana na tatizo hili Mhandisi Mchwampaka amesema kwa Chemba ya Migodi imehuisha hati yake ya makubaliano ya Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) ambapo hati hiyo imesainiwa mwezi Novemba 2023 ili kuanzisha kozi mpya 6 kwa ajili ya kuwafundisha mafunzo mchundo wa kuendesha na kufanya matengenezo ya mashine za uchimbaji wa chini ya ardhi.
Naye, Makamu wa Rais wa Kampuni ya AngloGold Ashanti ukanda wa Afrika Simon Shayo ambaye pia mjumbe wa baraza la TCM na ameishukuru na kupongeza Wizara ya Madini kwa utayari wake wa kujadiliana na wadau wa sekta ya madini kwa kusema kwamba, hatua hiyo ni msingi wa kuelekea katika maboresho ya mazingira ya ufanyaji kazi na uwekezaji kwa ujumla na itaendelea kufanya sekta ya madini kuwa ni yenye tija kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.