DODOMA-Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewasilisha makadirio ya bajeti ya shilingi trilioni 1.77 kwa ajili ya utekelezaji vipaumbele vyenye miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja, vivuko, mizani na ukamilishaji viwanja vikubwa vya ndege.
Amesema, kati ya kiasi hicho cha fedha, shilingi bilioni 81.4 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 1.6 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Ameyasema hayo leo bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Mheshimiwa Bashungwa amesema, katika mwaka huo wa fedha, wizara inatarajia kutekeleza Mpango na Bajeti kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).
Aidha, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020, Mpango Mkakati wa Wizara (2021/22 – 2025/26), Ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25.