DAR-Young Africans Sports Club (Yanga SC) ya jijini Dar es Salaam imeendelea kudhirisha kuwa, usajili wa msimu huu haukuwa wa kubabaisha.
Ni baada ya kuachilia kichapo cha mabao 3-0 kwa warina asali, Tabora United FC katika mwendelezo wa michezo ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Mabingwa hao mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara wameibuka kidedea kupitia mtanange uliopigwa Mei 25,2024 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Joseph Gnadou Guede dakika ya 19 alianza kulipa bili kwa waajiri wake Yanga SC akifuatiwa na Maxi Mpia Nzengeli dakika ya 49.
Bao hilo la kipindi cha pili lilidumu kwa muda mrefu, ndipo Stephane Aziz Ki dakika ya 90' akahitimisha hesabu.
Mabao hayo matatu ambayo yamewezesha, Yanga SC kuvuna alama tatu, yanawawezesha kujiwekea kibindoni alama 77 kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania.
Ushindi ambao hauwezi kufikiwa tena na timu yoyote, kwani Azam FC ipo nafasi ya pili kwa alama 66 huku watani wao Simba SC wakiwa nafasi ya tatu kwa alama 66.
Tags
Habari
Ligi Kuu ya NBC
Michezo
Tabora United FC
Yanga SC
Young Africans SC
Young Africans Sports Club