NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo amesema,mwaka 2023, thamani ya shilingi dhidi ya sarafu za nchi washirika wakuu wa kibiashara iliendelea kuwa tulivu.
Ameyasema hayo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25.
Prof.Mkumbo amesema, ilikuwa tulivu licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika uchumi wa dunia, hususani utekelezaji wa sera ya fedha katika nchi zilizoendelea uliolenga kupunguza ukwasi katika kukabiliana na mfumuko wa bei.
Katika kipindi hicho, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,395.7 ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,314.5 mwaka 2022.
Aidha, thamani ya shilingi ilishuka kwa asilimia 3.5 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 0.2 mwaka 2022.
Vile vile, katika kipindi kilichoishia Desemba mwaka 2023, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,516.0 ikilinganishwa na shilingi 2,320.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2022, sawa na kupungua kwa thamani ya shilingi kwa asilimia 8.4 Desemba 2023 ikilinganishwa na asilimia 0.56 Desemba 2022.
"Kupungua kwa thamani ya shilingi kulichangiwa na hatua zilizochukuliwa na nchi zilizoendelea katika kukabiliana na mfumuko wa bei ikiwemo utekelezaji wa sera ya fedha yenye lengo la kupunguza ujazi wa fedha.
"Utekelezaji wa sera hiyo ulisababisha kupanda kwa viwango vya riba ya dola ya Marekani kutoka asilimia 3.78 Novemba 2022 hadi asilimia 5.5 Agosti 2023 na hivyo, kuvutia uwekezaji katika masoko ya fedha ya Marekani na kusababisha upungufu wa dola katika mataifa mengine."
Amesema,katika kuimarisha utulivu wa shilingi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua mbalimbali zilizowezesha kuongeza fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni, ikiwemo kuuza dola pamoja na kutekeleza sera ya fedha yenye lengo la kupunguza ukwasi wa shilingi.
Pia, amesema Serikali ilianzisha mkakakti wa kuimarisha sekta za uzalishaji na huduma ikiwemo kilimo, uvuvi, samaki, utalii, madini na nishati mwaka 2023 kwa lengo la kuongeza mauzo nje na mapato ya fedha za kigeni.