Acheni siasa za malumbano, hazileti maendeleo-Dkt.Biteko

📌Afanya mkutano wa hadhara na wananchi wa jimbo la Bukombe

📌 Amshukuru Rais, Dkt. Samia kwa fedha za maendeleo Bukombe

📌 Ahimiza maendeleo kwa wana Bukombe

📌 Asisitiza ustahimilivu katika siasa

GEITA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewataka wananchi wa jimbo hilo kuacha siasa za malumbano kwani hazileti maendeleo na badala yake wajikite katika kujiletea maendeleo.
Dkt.Biteko ameyasema hayo wilayani Bukombe Mkoa wa Geita wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Bukombe kwa mualiko wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita katika mkutano uliolenga kutathmini hali ya maendeleo kwenye jimbo hilo.
Dkt. Biteko amesema Wana Bukombe hawana mtu mwingine wa kuwaletea maendeleo isipokuwa wao wenyewe na kuongeza kuwa siasa za malumbano hazileti maendeleo bali zinayachelewesha hivyo amewasisitiza wananchi hao kufanya kazi kwa bidii.

Aidha, kuhusu uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, Dkt. Biteko amewahimiza Wananchi wa jimbo hilo kuchagua viongozi wanaofaa na wanaotokana na CCM ili kutocheleweshewa maendeleo na kuwaasa kuwa wajifunze kuushinda ubaya kwa wema.
Akizungumzia miradi ya maendeleo jimboni Bukombe Dkt. Biteko amesema ‘’napenda nimpongeze Mhe Rais kwa kutuletea fedha za kutosha takribani shilingi bilioni 79 katika mwaka mmoja tu kwa ajili ya maendeleo Wilaya ya Bukombe kwenye sekta ya Elimu, Afya pamoja na miradi mingine ya maendeleo."

Ameongeza kuwa, mwaka 2015 Wilaya ya Bukombe ilikuwa na vituo vya afya viwili na zahanati 4, mtandao wa barabara ulikuwa kilomita 256 tu, mtandao wa maji wilaya nzima ulikuwa chini ya asilimia 15 na hakukuwa na sekondari kwenye kata lakini sasa kuna shule mpya za sekondari 7, shule za msingi mpya 11, vituo vya kutolea huduma za afya 25 na mtandao wa barabara umefikia kilomita 1400 hivyo amewataka wananchi kutembea kifua mbele kwa maendeleo yaliyopo.

"Mnapofanya siasa msing’oe Bendera za chama kingine cha siasa na inapotokea kuna mtu anang’oa bendera zenu niambieni nitanunua nyingine, kwani bendera haipigi kura, haichagui wala haiombi kura bali ni kitambulisho kuwa hiki chama kipo hivyo hakuna sababu ya kuvunja undugu kwasababu ya vyama vya siasa kwani sisi sote ni ndugu."
Kwa upande wake Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka matokeo zaidi kuliko maneno na ndio maana ameagiza TAMISEMI kuhakikisha inakarabati miundombinu iliyoharibiwa na mvua na kuhakikisha watumishi wa Sekta ya Afya na Walimu wanapelekwa wilayani Bukombe kwa maslahi mapana ya wananchi pamoja na kuboresha maendeleo.

‘’Wananchi wa Bukombe mna bahati ya kuwa na kiongozi mchapakazi, mpenda maendeleo na mwenye kiu ya kuleta maendeleo hivyo mumuenzi kwa vitendo,"amesema Mhe. Durance.Mkutano huo wa hadhara ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Geita Mhe. Rose Busiga na Wenyeviti wa CCM Mkoa na Wilaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news