Ajali za ndege zilivyoua Marais, Makamu wa Rais na Mawaziri Wakuu

NA GODFREY NNKO

AJALI za ndege zimeendelea kusababisha vilio na simanzi kwa wananchi wengi duniani, hii ni kutokana na ajali za mara kwa mara ambazo zimesababisha viongozi wao kupoteza maisha.
Ajali ya ndege iliyosababisha kifo cha Rais wa Poland,Lech Kaczynski.(Picha France24).

Katika makala hii utapata kufahamu baadhi ya matukio ya miaka kadhaa na hivi karibuni ambayo yanahusisha ajali za ndege zilizoua viongozi mbalimbali wakiwemo marais na makamu wao, na mawaziri wakuu.

Ikumbukwe ajali nyingi za ndege za viongozi zimekuwa zikihusishwa na hali mbaya ya hewa, vikwazo, makosa ya kibinadamu, hujuma au ugaidi. 

Mbali na changamoto hizo, bado usafiri wa anga unaendelea kuwa muhimu zaidi katika zama hizi za Sayansi na Teknolojia katika kurahisisha safari za viongozi kadri wanavyotaka kusafiri katika kudumisha diplomasia baina ya nchi na nchi,jumuiya na mashirika ya maendeleo ya Kimataifa.Endelea;

Dkt.Saulos Klaus Chilima

Ndege ya kijeshi aliyokuwa akisafiria Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Malawi,Mheshimiwa Dkt.Chilima ilipoteza mawasiliano ya rada Juni 10,2024 majira ya saa 3 asubuhi kwa saa za huko, ilipokuwa ikijiandaa kutua huko Mazuzu Kaskazini mwa Malawi.

Wadhibiti wa ndege walikuwa wamemshauri rubani kurejea Lilongwe, mji mkuu wa nchi hiyo, lakini alama za ndege hiyo zilipotea na baadaye ikapatikana ikiwa imeanguka msituni karibu na Mazuzu.

Vikosi vya uokoaji vilitatizika kutafuta mabaki hayo kutokana na uoto mnene. Aidha, Juni 11,2024 Rais wa Malawi, Mheshimiwa Lazarus Chakwera wakati akihutubia taifa alisema kwamba kila mtu aliyekuwa ndani ya ndege hiyo amefariki.

Afisa wa juu wa jeshi,Paul Valentino Phiri aliwaambia waandishi wa habari kwamba shughuli za utafutaji na uokoaji zilidumazwa na hali ya ukungu kuzunguka msitu wa Chikangawa ambapo ilikuwa shida kuona vizuri.

Ebrahim Raisi

Usiku wa kuamkia Mei 20,2024 Rais wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran, Ebrahim Raisi (63) alifariki baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kutoka Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo kuanguka.

Ebrahim alikuwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje,Hussein Amirabdollahian pamoja na viongozi wengine ambao wote walipoteza maisha katika ajali hiyo wakitokea katika shughuli za kikazi mpakani mwa Iran na Azerbaijan.

Chanzo cha ajali hiyo ni mabadiliko ya hali ya hewa huku ikielezwa kuwa, helikopita hiyo ilipata ajali karibu na eneo la Jolfa, zaidi ya kilomita 600 kutoka Tehran karibu na mpaka na Azerbaijan.

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei alimteua Makamu wa Rais, Mohammad Mokhber kushika madaraka ya muda kabla ya uchaguzi ndani ya siku 50.

Pia, Ali Bagheri, aliyewahi kuwa mpatanishi mkuu wa nyuklia wa nchi hiyo, aliteuliwa kuwa kaimu Waziri wa Mambo ya Nje.

Matukio hayo mawili ndani ya mwaka huu kwa viongozi waliopo madarakani, ni mwendelezo wa taarifa mbaya katika historia ndefu ya majanga ya anga ambayo yamegharimu maisha ya viongozi wa ulimwengu tangu kuanza kwa safari za anga.

Sebastian Pinera

Rais wa zamani wa Chile, Sebastian Pinera, alifariki Februari 6,2024 wakati helikopta ya Robinson R44 ilipoanguka Ziwa Ranco eneo la Los Ríos, Kusini mwa Chile.

Pinera alikuwa mfanyabiashara na mwanasiasa wa Chile ambaye alihudumu kwa mihula miwili kama Rais wa Chile kati ya mwaka 2010 hadi 2014 na 2018 hadi 2022.

Ndiye Rais wa kwanza wa kihafidhina kuiongoza nchi hiyo tangu kumalizika kwa utawala wa kidikteta wa Jenerali Augusto Pinochet mwaka wa 1990.

Arvid Lindman

Historia inaonesha, moja ya matukio ya kwanza ya kiongozi anayehudumu au mkuu wa nchi kufa katika ajali ya ndege alikuwa Arvid Lindman, Waziri Mkuu wa Sweden ambaye ndege aina ya Douglas DC-2 aliyokuwa akisafiria iligonga nyumba huko Croydon, Kusini mwa London.

Chanzo cha ajali hiyo ya Desemba 9,1936 kinatajwa kuwa ni hali mbaya ya hewa iliyosababisha ukungu mzito.

Ikumbukwe,enzi ya usafiri wa anga ilipoanza wakati wa vita, viongozi zaidi na zaidi walianza kupaa angani kwa ziara za kidiplomasia ili kuimarisha misingi ya tawala zao duniani.

Jose Felix Estigarribia

Pia, Septemba 7, 1940, Rais wa Paraguay, Jose Felix Estigarribia alifariki katika ajali ya ndege mwaka mmoja tu baada ya kuchukua madaraka.

Rais huyo wa 34 wa Paraguay alikuwa kwenye ndege ya Potez 25.Yeye na mke wake walifariki katika ajali hiyo ya ndege walipokuwa safarini kutoka Altos kwenda San Bernardino.

Wladyslaw Sikorski

Miaka mitatu baadae, kwa maana ya mwaka wa 1943 Waziri Mkuu wa Poland, Wladyslaw Sikorski alifariki kwa ajali ya ndege.

Ni ajali ambayo ilitokea Julai 4, 1943, wakati B24C Liberator ilipoanguka ndani ya Mediterania muda mfupi baada ya kupaa kutoka Gibraltar.

Aidha,wakati teknolojia na usalama wa usafiri wa anga ukiendelea kwa kasi baada ya Vita vya Pili vya Dunia huku nchi nyingi zaidi zikianza kuanzisha vikosi vyao vya anga na meli za kibiashara za kiraia, hitilafu za kiufundi, hali mbaya ya hewa, na mchezo mchafu uliendelea kupoteza maisha.

Ramon Magsaysay

Mnamo Machi 17, 1957 Rais wa Ufilipino,Ramon Magsaysay alifariki baada ya ndege yake kuanguka kwenye Mlima Manunggal huko Cebu.

Nereu Ramos

Juni 16,1958 rais wa mpito wa Brazil, Nereu Ramos alifariki katika ajali ya ndege ya Cruzeiro karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Curitiba Afonso Pena.

Barthelemy Boganda

Machi 29, 1959 Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Barthelemy Boganda alifariki baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kulipuka angani huko Bangui.

Abdul Salam Arif

Aprili 13,1966 Rais wa Iraq,Abdul Salam Arif alifariki kutoka na ajali ya helikopta ambayo ilidaiwa chanzo ni kunaswa na radi.

Helikopta hiyo ya Iraqi Air Force de Havilland DH. 104 Dove 1, RF392 ilipata ajali Kusini mwa Iraq kilomita 10 kutoka Uwanja wa Ndege wa Basra Airport.

Rene Barrientos

Matukio kama hayo yalifuatia kifo cha Aprili 27, 1969, cha Rais wa Bolivia, Rene Barrientos katika ajali ya helikopta huko Arque.

Joel Rakotomalala

Waziri Mkuu wa Madagaska, Joel Rakotomalala naye alifariki katika ajali ya Julai 30, 1976.

Rakotomalala alikuwa katika helikopta ya Aérospatiale Alouette III wakati wa safari fupi na mkuu wa wafanyakazi Alphonse Rakotonirainy, mwezi wa mwisho wa uwepo wa Vikosi vya Wanajeshi wa Ufaransa huko Madagaska.

Dzemal Bijedic

Hali mbaya ya hewa ilichangia kifo cha Waziri Mkuu wa Yugoslavia, Dzemal Bijedic mnamo Januari 18, 1977 wakati Gates Learjet lilipoanguka kwenye mlima wakati wa theluji kali.

Jaime Roldos Aguilera

Beech Super King Air 200 FAE-723 ilipoanguka Mei 24,1981 na kusababisha kifo cha Rais wa Ecuador, Jaime Roldos Aguilera,wengi walisema chanzo kilikuwa hali mbaya ya hewa.

Ajali hiyo pia iliondoka na Waziri wa Ulinzi, Meja Jenerali Marco Subia Martinez wakati ndege hiyo waliyokuwa wamepanda na Rais ilipoanguka karibu na mpaka wa Peru.

Samora Machel

Oktoba 19, 1986 saa 9:20 usiku ndege Tupolev-134A yenye usajili C9-CAA, iliyokuwa imembeba Rais Samora Machel na watu wengine 43 ilianguka Mbuzini, karibu na mpaka wa Msumbiji na Afrika Kusini.

Machel na watu wengine 33 walifariki katika ajali hiyo huku watu tisa akiwemo Mrusi walinusurika huku chanzo kikitajwa ni hali mbaya ya hewa.

Humberto de Alencar Castelo Branco

Vile vile,kadiri anga lilivyozidi kuwa na shughuli nyingi, uwezekano wa ajali uliongezeka.

Mnamo Julai 18, 1967, Humberto de Alencar Castelo Branco, rais wa kwanza wa kijeshi wa Brazil baada ya mapinduzi ya 1964 alifariki katika mgongano wa anga wa ndege ya Piper PA-23 karibu na Fortaleza.

Ahmed Ould Bouceif

Mnamo Mei 27, 1979, Ahmed Ould Bouceif, Waziri Mkuu wa Mauritania alifariki katika ajali ya ndege kwenye pwani ya Dakar, Senegal.

Francisco Sa Carneiro

Naye Francisco Sa Carneiro ambaye alihudumu kama Waziri Mkuu wa Ureno kwa miezi 11 pekee alifariki Desemba 4,1980.

Omar Torrijos

Kiongozi wa Panama, Jenerali Omar Torrijos alifariki Julai 31, 1981, wakati ndege yake ya Jeshi la Wanahewa la Panama ilipoanguka katika mazingira ya kutiliwa shaka.

Rashid Karami

Mnamo Juni 1, 1987, mwanasiasa wa Lebanon Rashid Karami, ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu mara nane, aliuawa wakati bomu lilipolipuka kwenye helikopta yake muda mfupi baada ya kupaa kutoka Beirut.

Juvenal Habyarimana na Cyprien Ntaryamira

Miongoni mwa matukio ya kusikitisha sana ni Rais wa Rwanda, Juvenal Habyarimana na Rais wa Burundi, Cyprien Ntaryamira wote waliuawa Aprili 6, 1994, wakati Dassault Falcon 50 9XR-NN ilipodunguliwa walipokuwa wakikaribia uwanja wa ndege wa Kigali nchini Rwanda.

Zia Ul-Haq

Kumekuwa na chunguzi kadhaa kuhusu ajali ya ndege iliyomuua Jenerali Zia Ul-Haq wa Pakistan Agosti 17, 1988.

Aidja,hakuna sababu ya kuridhisha iliyopatikana, na kusababisha msururu wa nadharia za mauaji huku maswali yakiwa mengi.

Ndege ya Jeshi la Anga la Pakistani Lockheed C-130B ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka Bahawalpur.

Kwa mujibu wa wachunguzi, ndege hiyo ilianguka kutoka angani na kugonga ardhi kwa nguvu kiasi kwamba ililipuliwa vipandevipande na mabaki ya ndege kusambaa katika eneo kubwa.

Licha ya maboresho makubwa katika usalama wa anga, misiba imeendelea kutokea hadi kufikia milenia mpya.

Boris Trajkovski

Februari 26, 2004 Rais wa Masedonia, Boris Trajkovski alifariki wakati ndege yake aina ya Beechcraft Super King Air 200 Z3-BAB ilipoanguka ilipokuwa ikijaribu kutua katika hali mbaya ya hewa huko Mostar.

John Garang

Katika hatua nyingine John Garang, kiongozi wa Sudan People’s Liberation Army na kwa muda mfupi makamu wa kwanza wa rais wa Sudan, alifariki dunia wakati helikopta yake ilipoanguka kwenye safu ya milima Kusini mwa nchi hiyo.

Ni baada ya kukabiliwa na hali mbaya ya hewa Julai 30, 2005.

Muhammadu Maccido

Oktoba 29, 2006 Muhammadu Maccido, sultani wa Sokoto nchini Nigeria alifariki pamoja na mwanaye wakati ndege yake ya ADC Airlines Flight 53 ilipoanguka.

Lech Kaczynski

Rais wa Poland,Lech Kaczynski alifariki Aprili 10, 2010 katika ndege ya Tupolev-154 ilipoanguka kutokana na hali mbaya ya hewa
wakati inakaribia uwanja wa ndege wa Smolensk magharibi mwa Urusi.(NA/DIRAMAKINI)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news