Anayetaka kunikera anikanyagie uchumi wangu, Mchechu songa mbele-Rais Dkt.Samia

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amemtaka Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu kufanya kazi kwa bidii bila kujali sifa kutoka kwa mtu yeyote.
"Kwenye mageuzi haya, Mchechu na Waziri wako lazima muwe unpopular, lazima muwe unpopular kama vile sijawahi kusikia Waziri wa Fedha akisifiwa hata siku moja, siku zote Waziri wa Fedha analaaniwa."

Mhesimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Juni 11,2024 katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka wakala,taasisi,mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo, Rais Samia amepokea gawio na michango kutoka kwa mashirika 145 yenye thamani ya jumla ya Shilingi 637,122,914,887.59 ikijumuisha gawio Shilingi 278,868,961,122.85 kutoka katika Mashirika ya Biashara na michango Shilingi 358,253,953,764.74 kutoka katika taasisi nyingine.
"Kwa hiyo Mchechu na wewe utalaaniwa tu hapa,lakini hii ndiyo kazi niliyokupa fanya. Ndiyo kazi niliyokupa simama na uifanye.

"Mageuzi haya, lazima yaendelee, mageuzi aliyoyasema Msajili wa Hazina kwenye mashirika na kwa sababu ni mashirika ya umma, mashirika ya Serikali hakuna anayeweza kupiga haya mageuzi.

Kwamba huku kwangu mimi sitaki hiki kije. Hapana, lazima twende na mageuzi haya."

Vile vile, Mheshimiwa Dkt.Samia ameendelea kuwataka viongozi wa wizara ambazo zina mashirika kuacha kuweka mikono na maelekezo ya kutaka fungu.

"Lakini niseme kwamba, viongozi wa wizara ambao mna mashirika, nasema leo mara ya pili, nadhani nilizungumza kule Arusha kwenye kile kikao cha retreat kwamba, viongozi wa wizara acheni kutia mikono huko na kupeleka meseji nyingi, fanya hili, fanya lile.

"Leta...nadhani bado yanatokea kwa sababu bado wanapiga makofi (washiriki wakipiga makofi na kufurahi)."

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Dkt.Samia ameendelea kusisitiza ubunifu katika mashirika ya umma ili kuleta tija.

"Lakini, muwaruhusu wawe na ubunifu, nilikuwa ninaangalia wanaokuja kuleta cheki hapa, ni vijana wadogo wadogo na hata wenyeviti hauwezi kumuita Mzee naye bado kijana.

"Kwa hiyo vijana hawa wana ubunifu, waacheni,wapeni fursa watumie ubunifu wao kuangalia vyanzo vya fedha, kuangalia nini watafanya ili waweze kukuza mashirika yao.

"Mnajua ninyi mliopewa dhamana ukiweza kulikuza shirika ni legacy yako kwamba umefanya, umeweza.

"Wenyeviti au watendaji ni legacy yenu na inakupa furaha ya moyo wako kwamba umefanya, umeweza na shirika lazima ulisimamie kama la kwako.

"Sasa, ninaposema hivyo, watu mnakwenda kulisimamia shirika kama la kwenu,mnaweka fedha mfukoni na kufanya mnavyotaka siyo kufuata miongozo ya Serikali kuongeza shirika pato la shirika, kuongeza pato la shirika ili Serikali ipate na ninyi kama viongozi wa shirika na watendaji muweze kupata pia.

"Kwa sababu mkisema mnamkamua Mama Serikali kila mwaka, sisi tunatoa, ninyi hamrudishi, hiyo ni biashara kichaa na mtu yeyote mwenye akili hiyo biashara haielewi.

Kwamba wewe unapokea tu, haurudishi kitu na muongozo wako kwenye shirika unakuambia kabisa kwamba wewe ufanye kitu.

Kwa hiyo, yale mashirika ambayo mnatoa huduma tunayaelewa, tunayaelewa vizuri sana,kwa hiyo angalau muwe na mzigo wa yale yanayotoa huduma na yale ambayo yanafanya biashara mjikongoje mje juu mpate na Serikali ipate mtupunguzie mzigo.

Rais Dkt.Samia amesema kuwa, katika hatua za kupata mageuzi ya kiuchumi wapo baadhi ya watu watakaokanyagwa ambao wataonesha kutokwenda mbele.
"Katika mageuzi haya tutawakanyaga watu wengi sana wale ambao hawataki kwenda mbele na ndio watakaopiga kelele nyingi sana..sasa ndugu yangu wewe, mwanangu wewe uliye kwenye shirika ambaye hutaki kukanyagiwa nguru wako nenda kachape kazi.

"Leteni mageuzi, chapeni kazi kwenye mashirika ili tuone tija ikionekana basi hatutakanyaga nguru wako, lakini kama utataka kunikanyagia mimi nguru wangu wa uchumi..aaah na mimi nitamkanyaga wako.

"Tufanye kazi ili tulete tija kwa Taifa, makelele tusiyasikilize, tupande mti kisha tukishuka tutawauliza mnasemaje."

Katika hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema,sheria inayosimamia Ofisi ya Msajili wa Hazina inaelekeza mashirika kutumia si zaidi ya silimia 60 ya mapato yake iliyoyakusanya na kutoa gawio kwa serikali ambapo hadi sasa zaidi ya taasisi 145 zimetoa huku 159 zikitarajiwa kutoa kati ya 304.

Mchechu ameongeza kuwa, taasisi zote zimeingia mkataba wa utendaji kazi kati ya bodi zao na ofisi ya Msajili wa Hazina na kwamba wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kuripoti taarifa za utendaji wa watendaji wa wakuu wa taasisi.
Amesema,hadi kufikia Mei 2024 ofisi yake ilikuwa imepokea gaewio la shilingi bilioni 637 ambapo shilingi bilioni 279 kutoka ya mashirika ya biashara na shilingi bilioni 358 ni taasisi za umma.

“Lengo letu ni kupokea gawio shilingi bilioni 850, ila kwa sasa tumepokea shilingi bilioni 637 kutoka taasisi 149 kati 159 imani yetu hadi mwisho wote watatoa."

Wakati huo huo, Rais Dkt.Samia amesema, Serikali inaweka mazingira bora ya kufanya biashara, kutunga sera rafiki zinazohamasisha uwekezaji nchini kwa nia ya kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za jamii.

Amesema, upokeaji gawio ni ishara kuwa mazingira yaliyowekwa yanafanya kazi na kuwezesha kupatikana kwa fursa ya kufanya biashara na kupata faida.

Pia ametoa wito kwa viongozi wa Mashirika yote ambayo bado hayajatoa mchango wake kwa Serikali, na yale ambayo yametoa chini ya kiwango wanachotakiwa kutoa, kuhakikisha wanafanya hivyo kabla ya Mwaka wa Fedha wa 2024 haujaisha.
Rais Dkt.Samia amesema kuwa, ataendelea kusimamia mageuzi katika uendeshaji wa Mashirika ya Umma ili kuyawezesha kujiendesha kibiashara na kwa tija zaidi kwa manufaa ya Watanzania.

Hata hivyo, ameelekeza mashirika kufikia mwezi Desemba 2024 kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana kama walivyofanya Shirika la Mapato nchini (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news