RUVUMA-Godfrey Eusebius Luoga ambaye ni Askari Mgambo amelipa faini ya shilingi 500,000 kwa kosa la kupokea hongo ya shilingi 20,000.
Hukumu hiyo imetolewa leo Juni 24, 2024 kupitia Kesi ya Jinai Na.17135/2024 mbele ya Mheshimiwa Lilian Ernest Rugarabamu (PRM), Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Katika shauri hilo lililoendeshwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwinyi Yahaya, Mshtakiwa huyo alishtakiwa kwa kosa la kupokea hongo ya sh. 20,000.
Ikiwa ni kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Sura ya 329 Mapitio ya Mwaka 2022) kutoka kwa mwananchi Mohamedy Faraji Ponera.
Lengo lilikuwa ni ili asimkate kutokana na kutochangia mchango wa chakula cha shule kwa mtoto wake anayesoma Shule ya Msingi Lipokela iliyopo Halmashauri ya Wilaya Songea mkoani Ruvuma.
Mahakama imemhukumu kulipa faini ya shilingi 500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Hata hivyo, mshtakiwa amelipa faini jumla ya shilingi 500,000.