Bangi inaweza kukufanya kuwa kichaa-Dkt.Mfisi

NA GODFREY NNKO

KWA mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya nchini (DCEA),bangi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa Cannabis sativa.
Mmea ambao hustawi na hutumika kwa wingi hapa nchini na duniani kote.

Aidha,bangi huathiri ubongo na kubadili jinsi tunavyotafsiri uhalisia wa vitu. Majani na maua ya mmea huo hukaushwa na hutumiwa kama kilevi peke yake au kwa kuchanganywa na dawa zingine.

Mara nyingi bangi imekuwa ni kati ya dawa ya awali kutumiwa, ambapo watumiaji wengi huanza matumizi wakiwa na umri mdogo hivyo kuwa katika hatari zaidi kiafya, kijamii na kiuchumi.

Vile vile, watumiaji wengi wa bangi huishia kutumia dawa nyingine hapo baadae kama heroin na cocaine.

Hivyo, bangi hutumika kama njia ya kuingia katika matumizi ya dawa nyingine za kulevya.

Kamishina wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Dkt. Peter Mfisi katika mahojiano na Redio One hivi karibuni jijini Dar es Salaam amebainisha kuwa, matumizi ya bangi yanaweza kumfanya mtu kuwa kichaa.

"Bangi inaharibu mfumo wa fahamu kabisa, kwa hiyo mtu anaweza hata akawa na changamoto ya afya ya akili, kwa neno ambalo tumelizoea tunahita kichaa, anaweza akawa.

"Ukichukua watu 100 wanaovuta bangi, halafu ukachukua watu 100 wanaovuta sigara unaweza usipate mtu hata mmoja anayepata kichaa anayevuta sigara,lakini unaweza ukakuta watu 90 wanaovuta bangi wanapata kichaa.

"Ninatumia neno kichaa ingawa halitumiki sasa hivi kwa ajili ya uelewa wa binadamu, kwa sababu ukimuambia mtu anapata changamoto ya afya ya akili anajua ni kawaida tu.

"Watu wachache tunaoelewa, tunajua changamoto ya afya ya akili ni nini, unapotumia neno kichaa ni neno la kinyanyapaa, lakini tunapotaka kukataza kitu lazima tulitumie ili kuhakikisha watu hawaingii kwenye matumizi.

"Maana yake madaktari watakuja kunilaumu kwamba kwa nini umetumia neno la kinyanyapaa, ninasema hivi ili kuleta uelewa kwa jamii, kwamba ukisema kichaa jamii inaelewa kwa uzito unaotakiwa.

"Kuliko kusema anapata changamoto ya afya ya akili, changamoto ya afya ya akili ni kama kusema hata mtu anaweza kupita hajachana nywele, anaweza kuwa na changamoto ya afya ya akili.

"Kwa hiyo, kutumia maneno mazito ni ili watu wasifananishe bangi na sigara ila sisi tunawakataza watu kuvuta sigara kwa sababu sigara ndiyo lango la kuingia kwenye matumizi ya bangi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news