Benki kuu EAC zinawajibu huu, abainisha Naibu Gavana Msemo

ARUSHA-Kikao kazi cha 17 kinachofanya tathmini ya uthabiti wa sekta ya fedha kwa kuzingatia vihatarishi vinavyoikumba sekta ya fedha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kimeanza jijini Arusha.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Bi. Sauda Msemo, amesema kikao hicho ni muhimu kwa mfumo wa kifedha na uchumi wa EAC, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia changamoto mbalimbali za kiuchumi.
“Kikao hiki kitaboresha udhibiti wa vihatarishi katika ukanda wa EAC kwa ajili ya kuimarisha uthabiti wa Sekta ya Fedha. Hii inawezekana kupitia kutambua, kuchambua na kuripoti mapendekezo kwa Kamati ya Masuala ya Fedha ya EAC (MAC), kwa ajili ya kupata mwongozo ili kutengeneza mfumo imara wa kifedha,” amesema Bi. Msemo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Meneja, Idara ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Edista Njau.
Aliongeza kuwa benki kuu zilizopo katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zina wajibu wa kutatua changamoto zilizopo katika ukanda huo zinazohatarisha uthabiti wa sekta ya fedha.

“Ili kuhakikisha EAC haibaki nyuma, benki kuu zilizopo katika Jumuiya hii, zina wajibu wa kuweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto zinazohatarisha uthabiti wa sekta ya fedha katika ukanda wetu, zikiwemo changamoto za kifedha zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, vihatarishi vya mtandaoni na teknolojia ya huduma za fedha,” ameeleza.
Nao, washiriki wa mkutano huo wamesema kikao hicho kinatoa fursa kwa benki kuu zilizopo katika ukanda wa EAC kujadili changamoto na vihatarishi mbalimbali vinavyoikumba sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla.

Kikao hicho kinachofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha kuanzia tarehe 17 hadi 21 Juni, 2024 ni cha kwanza kuhudhuriwa na Benki Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (BCC) kufuatia nchi hiyo kujiunga na EAC hivi karibuni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news