DODOMA-Katika kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 58 tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wafanyakazi wa Makao Makuu ya BoT Dodoma wametoa misaada kadhaa kwa vituo vya watu wenye mahitaji maalum katika wilaya za Kondoa na Kongwa tarehe 14 Juni,2024.
Wakiongozwa na Meneja Uendeshaji, Bw. Nolasco Maluli katika Kituo cha Poloni Orphans House huko wilayani Kondoa, wafanyakazi wa Benki Kuu wametoa mchele, mafuta ya kupikia, unga wa ngano, maharage, unga wa ugali, gesi ya kupikia, madaftari, mashuka, mablanketi na magodoro.
Meneja Msaidizi Utawala na Fedha, Bi. Maristella Kamuzora, aliongoza ujumbe wa Benki Kuu katika Kituo cha Watoto Wenye Ulemavu wa Viungo Mlali wilayani Kongwa na kuwapatia mchele, mafuta ya kupikia, unga wa ngano, maharage, unga wa ugali, mafuta ya kupakaa, mablanketi, vitimwendo (vitimaguru) kwa ajili ya watoto, soksi za kushindia, tracksuits, poti za watoto na masweta kwa ajili ya baridi.