NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba amesema, benki zinazomilikiwa na Serikali ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB) na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) zimeendelea kuonesha ufanisi mkubwa katika soko la fedha nchini.
Ameyasema hayo leo Juni 4, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.
TADB
Amesema, katika mwaka 2023, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilipanga kuzalisha mapato ya shilingi bilioni 45.10.
Vile vile, kukuza faida ya benki kabla ya kodi ya shilingi bilioni 18.50, kutoa mikopo ya shilingi bilioni 120, thamani ya mali za benki kufikia shilingi bilioni 562.70 na kufuatilia urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wateja shilingi bilioni 62.
Waziri Dkt.Nchemba amesema, hadi Desemba 2023, benki ilikusanya mapato ya jumla ya shilingi bilioni 41.56, sawa na asilimia 92.15 ya lengo na kutengeneza faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 18.79, sawa na asilimia 107.9 ya lengo.
Aidha, benki ilitoa mikopo ya shilingi bilioni 161.60, sawa na asilimia 134.67 ya lengo na thamani ya mali ilifikia shilingi bilioni 606.94, sawa na asilimia 107.86 ya lengo.
Dkt.Nchemba amesema,benki ilifuatilia urejeshaji wa mikopo ya shilingi bilioni 92.0 sawa na ufanisi wa asilimia 148.4 ya lengo.
TIB
Katika mwaka 2023, Waziri Dkt.Nchemba amesema, Benki ya Maendeleo TIB ilipanga kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 11.62 kwa miradi ya maendeleo kwenye sekta ya maji, nishati na uongezaji thamani mazao ya kilimo.
Pia, kukusanya shilingi bilioni 41.69 kama marejesho ya mikopo kutoka kwa wateja na kukusanya shilingi bilioni 7.39 ikiwa ni marejesho ya mikopo iliyoshindikana na kuondolewa kwenye mizania ya benki.
Amesema, hadi Desemba 2023, benki ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 9.74, sawa na asilimia 83.82 ya lengo.
Aidha, benki hiyo ilipokea marejesho ya mikopo ya shilingi bilioni 42.63 sawa na asilimia 102.30 ya lengo.
"Vilevile, benki ilikusanya shilingi bilioni 6.51 kutoka kwa wateja kama marejesho ya mikopo iliyoshindikana na kuondolewa kwenye mizania ya benki, sawa na ufanisi wa asilimia 88.09 ya lengo."
TCB
Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, katika mwaka 2023, Benki ya Biashara Tanzania ilipanga kuzalisha mapato ya shilingi bilioni 184.2.
Ikiwemo kukuza faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 12.4, kutoa mikopo ya shilingi bilioni 904, kukusanya amana za wateja shilingi bilioni 1,121 na kukuza mali za benki kufikia shilingi bilioni 1,446.
Jambo lingine ni kukuza mtaji kufikia shilingi bilioni 123.8 na kuunda mfumo wa kielektroniki wa tathmini na ufuatiliaji wa mwenendo wa mikopo.
"Hadi Desemba 2023, mapato ya benki yalifikia shilingi bilioni 192.1, sawa na asilimia 104.3 ya lengo, mikopo iliyotolewa ilifikia shilingi bilioni 911.2 sawa na asilimia 100.8."
Waziri Dkt.Nchemba amesema, amana zilifikia shilingi bilioni 1,120.7 sawa na asilimia 99.9 ya lengo huku mtaji wa benki ukifikia shilingi bilioni 118.9 sawa na asilimia 96 ya lengo.
Amesema,benki ilikuza mali kufikia shilingi bilioni 1,389.3 sawa na asilimia 96.1 ya lengo. Aidha, benki ilipata hasara ya shilingi bilioni 44.4 kabla ya kodi 39 kutokana na kufutwa kwa mali chechefu iliyorithiwa ya shilingi bilioni 54.4 kutokana na kuunganishwa na benki nyingine tatu.
Waziri Dkt.Nchemba amesema, mfumo wa kielektroniki wa tathmini na ufuatiliaji wa mwenendo wa mikopo unaendelea kusimikwa kufungamanishwa na mifumo mingine ya benki.