NA GODFREY NNKO
SERIKALI imesema kuwa, mwaka 2023, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliendelea kutekeleza sera ya fedha kwa lengo la kupunguza ongezeko la ukuaji wa ukwasi katika uchumi.
Pia, kudhibiti mfumuko wa bei uliotokana na kupanda kwa bei za bidhaa katika soko la dunia na kuendelea kuchangia ukuaji wa uchumi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo ameyasema hayo leo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25.
"Katika kipindi hicho, ukuaji wa ujazi wa fedha ulikuwa sambamba na mahitaji ya shughuli za kiuchumi ambapo ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 14.1 na kufikia shilingi bilioni 44,002.6 mwaka 2023 kutoka shilingi bilioni 38,580.0 mwaka 2022."
Amesema, ongezeko hilo lilitokana na ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. Aidha, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana (M2) ulikua kwa asilimia 11.9 na kufikia shillingi bilioni 34,001.7 mwaka 2023 kutoka shilingi bilioni 30,378.9 mwaka 2022.
Vile vile, ujazi wa fedha kwa tasfiri finyu (M1) uliongezeka kwa asilimia 8.7 na kufikia shilingi bilioni 20,601.6 mwaka 2023 kutoka shilingi bilioni 18,948.2 mwaka 2022.