DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inashirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya huduma ndogo za fedha nchini, hususani huduma za mikopo, ili kuiwezesha sekta hiyo kuwa na manufaa kwa wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla.


Gavana ameeleza kuwa,mikopo mingi inatozwa gharama kubwa zisizoeleweka kama vile ada ya fomu, ada ya kushughulikia mkopo, na ada ya mkopo.
Amwsema,mwongozo mpya utakaotolewa utadhibiti gharama hizo zote ziwe sehemu ya ada ya mkopo pekee.
"Kuna baadhi ya wakopeshaji wanaweka riba na gharama za bima zisizoeleweka, lakini miongozo itadhibiti gharama za ziada zisiwe sehemu ya mkopo. Pia, watatakiwa kuwasilisha viwango vyao vya riba BoT kwa ajili ya kuviidhinisha na vitatumika kwa mwaka mzima," ameongeza.
Kwa upande wa wakopaji, Gavana amesema kuwa changamoto kuu ni kutokurejesha mikopo kwa wakati, huku wakopeshaji wakikosa uwazi wanapokosesha.
“Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma, ikiwemo kuingiza mada za elimu ya fedha katika mitaala rasmi ili kuhakikisha watu wanapohitimu shule wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha,”alisema.
Gavana Tutuba amesisitiza kuwa, BoT inaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wanaokiuka sheria, ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya leseni na kuwapeleka mahakamani.
Akiwasilisha mada kuhusu mfumo wa Sera ya Fedha unaotumia riba, Meneja Msaidizi, Kurugenzi ya Utafiti na Sera za Uchumi BoT, Dkt. Lusajo Mwankemwa, amesema kuwa kuanzia Januari 2024, Benki Kuu imeanza kutoa mwelekeo wa riba itakayotumika katika soko la fedha baina ya mabenki, badala ya kutumia ujazi wa fedha.

“Mabadiliko katika riba hiyo yanaashiria mwelekeo wa Sera ya Fedha katika kuhakikisha kuwa ukwasi katika Uchumi unaendana na malengo ya kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa Uchumi,”amesema.
Dkt. Mwankemwa ameongeza kuwa, mfumo wa kutumia riba katika kutekeleza Sera ya Fedha ni miongoni mwa mifumo inayotumika kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa Uchumi. Ili mfumo huu uweze kuleta ufanisi katika kufikia malengo yaliyokusudiwa, ni muhimu kufanya kazi pamoja na sera nyingine za Uchumi.