BoT yaendesha mkutano wa udhibiti wa majanga EAC

ARUSHA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaendesha mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaolenga kujadili udhibiti wa majanga (Crisis Management) kwa nchi za EAC.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Bi. Sauda Msemo, amesema mkutano huo ni muhimu katika mfumo wa kifedha na uchumi wa EAC, hususan kipindi hiki ambacho dunia inapitia changamoto mbalimbali za kiuchumi.

"Mkutano huu ni sehemu muhimu ya jitihada za Kamati ya Kujadili Masuala ya Fedha (MAC) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo tunajiunga kwa pamoja kuimarisha utulivu wa sekta ya fedha, maandalizi ya kukabiliana na majanga, usimamizi na mikakati ya kutatua changamoto katika jumuiya yetu kwa kushirikiana na kubadilishana uzoefu,” amesema Bi. Msemo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Meneja Uendeshaji wa Bodi ya Bima ya Amana, Bw. Nkanwa Magina.
Aliongeza kuwa, magavana wa Benki Kuu katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamelipa kipaumbele suala la kuweka mikakati sahihi ya kukabiliana na majanga katika sekta ya fedha ili kuhakikisha utulivu wa sekta hiyo.

"Katika mkutano wa 27 wa Kamati ya Masuala ya Fedha (MAC), magavana wa Benki Kuu ukanda wa Afrika Mashariki walijadili umuhimu wa kuwa na hatua za pamoja za kushughulikia majanga katika sekta ya fedha. Hatua hizi ni pamoja na kuhakikisha benki na taasisi za fedha zinaandaa mipango ya kurejesha shughuli za taasisi wakati wa majanga (recovery plan) ili kuruhusu mwendelezo wa shughuli za kifedha na kiuchumi katika nyakati hizo," ameeleza.

Mkutano wa mwaka huu unaofanyika tarehe 10 hadi 14 Juni 2024 ni wa kwanza kuhudhuriwa na Benki Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (BCC) kuhudhuria.

Akiongea katika mkutano huo, Bw. Emmanuel Kalala kutoka Idara ya Usimamizi wa Mabenki BCC, amesema mkutano huo umewapa fursa ya kubadilishana uzoefu na washiriki wengine kuhusiana na mipango ya kurejesha shughuli za taasisi yao pindi majanga yanapotokea.
Aidha, wameweza kushirikishana miongozo mbalimbali ambayo mabenki na taasisi nyingine za fedha zinapaswa kuwa nayo ili kuleta utulivu katika sekta ya fedha nchini Congo na katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news