BoT yaja na Mambo ya Fedha:Ujanja Pesa-Kujiajiri Inawezekana kupitia Clouds Media

DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT)imezindua mradi wa elimu ya fedha kupitia Clouds Media, unaojulikana kama "Mambo ya Fedha: Ujanja Pesa - Kujiajiri Inawezekana" ambao ni sehemu ya mkakati mpana wa BoT wa kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wananchi wote, mijini na vijijini, kuanzia watoto hadi wazee.
Katika uzinduzi huo uliofanyika leo Juni 27,2024 kwenye ofisi za BoT jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema mradi huu umelenga kuwawezesha wananchi kwa kutoa elimu kuhusu usimamizi binafsi wa fedha.

"Benki Kuu imeingia makubaliano na Clouds Media ya kuitambua kama chombo cha habari kinachoweza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi kwa kuzingatia mwongozo wa wakufunzi wa elimu ya fedha tuliouzindua mwaka jana,”amesema Gavana Tutuba katika hotuba iliyosomwa na Naibu Gavana, Dkt. Yamungu Kayandabila.

Aidha, Benki Kuu pia imeingia makubaliano na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu hapa nchini, ikiwemo Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), ambacho kitakuwa kinawafundisha na kuwathibitisha wanahabari wa Clouds FM kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi.“Takwimu za utafiti wa Fincap zinaonesha kwamba chini ya asilimia 40 ya wananchi wanaelewa na kumudu usimamizi binafsi wa fedha. Mradi huu ni sehemu ya jitihada za kutatua changamoto hii na kuboresha ujumuishi wa huduma rasmi za fedha kwa wananchi."

Dkt. Kayandabila alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kufikisha elimu ya fedha kwa wananchi, hususan kupitia mradi huu wa Clouds Media. "Kwa kupitia vyombo vya habari, tunatarajia kufikia makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo vijana, wanawake, wazee, na wale walioko nje ya mifumo rasmi ya fedha.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Miradi Maalum kutoka Clouds Media, Bw. Samsonite Odera, Amesema kuwa utelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kuwawezesha wananchi kuanzisha miradi mbalimbali yakuwaingizia kipato, utahusisha mikoa 31 nchini kwa kufanya matamasha, mikutano na michezo mbalimbali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Mpango huu ni sehemu ya "Mpango Mkuu wa Sekta ya Fedha 2020-2030" chini ya Wizara ya Fedha, na "Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha 2023-2028" ulio chini ya Baraza la Huduma Jumuishi za Fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news