BoT yawakutanisha wanahabari mikoa saba kuwajengea uelewa masuala ya uchumi

DODOMA-Katika juhudi za kuimarisha uelewa wa waandishi wa habari kuhusu majukumu na masuala ya uchumi na fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeandaa semina maalum kwa waandishi wa habari kutoka mikoa saba ya Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Morogoro, Iringa, na Njombe.
Semina hiyo ya siku tatu inayowashirikisha waandishi wa habari 40 inalenga kujenga uwezo wa waandishi hao kuripoti kwa usahihi na ufanisi zaidi masuala ya uchumi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Meneja Idara ya Uendeshaji Tawi la BoT Dodoma, Bw. Nolasco Maluli, alibainisha kuwa utaratibu wa kukutana na waandishi wa habari umekuwa ukifanyika kwa zaidi ya miaka 12, ambapo umesaidia waandishi kupata ufafanuzi wa kina wa masuala mbalimbali ya uchumi na fedha na kuwawezesha kutoa habari kwa ufasaha kwenye vyombo vya habari.
"Tumeshuhudia kuboreshwa kwa kazi zinazofanywa na waandishi wa habari, ikiwemo kututafuta pale wanapohitaji ufafanuzi wa kina wa masuala mbalimbali," alisema Bw. Maluli. Aliongeza kuwa kwa miaka ya hivi karibuni, Benki Kuu imekuwa ikisikika sana kwenye vyombo vya habari na kwa sehemu kubwa kwa usahihi.

Mada kuu katika semina hiyo ni kuhusu Majukumu ya Benki Kuu, Mfumo mpya wa Sera ya Fedha ya kutumia Riba ya Benki Kuu, utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, uwekezaji katika Dhamana za Serikali, na alama za usalama katika fedha pamoja na utunzaji mzuri wa noti na sarafu. Mada hizo zinatarajiwa kutoa uelewa mpana kwa waandishi wa habari na kuwasaidia kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vyao vya habari.Awali, Meneja Idara ya Mawasiliano BoT, Bi. Victoria Msina, amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa kuwa sehemu muhimu sana kwa Benki Kuu kuweza kuwafikia wananchi kupitia taarifa mbalimbali wanazozitoa, zikiwemo habari, makala, mahojiano, na vipindi maalum vya masuala yanayohusu uchumi, biashara na fedha.

"Tunafarijika sana kwa kuwa mmekuwa daraja muhimu kati ya Benki Kuu na wananchi," alisema.

Semina hiyo inatarajiwa kuleta matokeo chanya katika uboreshaji wa uandishi wa habari za uchumi na fedha nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news