DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila, amesema mafunzo ya elimu ya fedha kwa wanaotoa elimu hiyo yatawasaidia wananchi kupata elimu sahihi na yenye ubora kuhusu matumizi ya fedha zao ili kujikwamua kiuchumi.

“Tunaamini kuwa elimu na maarifa mliyopata kupitia mafunzo haya si kwa ajili ya maendeleo yenu binafsi tu, bali pia itakwenda kuwasaidia wananchi walio wengi, ambao hawana uelewa mzuri juu ya elimu ya fedha,” amesema Dkt. Kayandabila.
Aidha, ameongeza kuwa mafunzo hayo yatakuwa endelevu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za teknolojia zinazokumba ulimwengu.

“Tutahimiza watoa huduma za fedha waweke vikokotoo vitakavyowasaidia walaji kupiga hesabu za mikopo yao vizuri,” amesisitiza Dkt. Kayandabila.
Naye, Meneja wa Huduma Jumuishi za Fedha Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Nangi Massawe, amesema mafunzo hayo yatasaidia kutokomeza vitendo vinavyofanyika kinyume na taratibu katika sekta ya fedha.

“Tunatarajia kuwa na umma ulioelimika ili vitendo visivyo vya haki katika sekta ya fedha kama vile viwango vya juu vya riba, mikopo isiyolipika, udanganyifu, uhalifu wa mtandao, utakatishaji fedha na ukosefu wa uwajibikaji kwa watoa huduma za fedha vikose nafasi katika jamii,"amesema.
Akiongea kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo hayo, Bw. Mark Peter, amesema, wao kama wahitimu wa kundi la kwanza wa mafunzo hayo, wameazimia kutoa elimu ya fedha kwa umma kwa weledi na umahiri sawasawa na sera, kanuni, mtaala na miongozo waliyopewa na serikali kupitia Benki Kuu.