DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Taasisi ya Malipo ya Taifa ya India (National Payment Corporation of India), inayosimamiwa na Benki Kuu ya India kwa lengo la kujadiliana fursa za ushirikiano kwenye mfumo wa kidijitali wa malipo.
Akizungumza katika mkutano huo, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba,ambaye alishiriki kwa njia ya mtandao, aliueleza ujumbe huo kuwa Benki Kuu ilizindua Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Hapo, yaani Tanzania Instant Payment System (TIPS) mwezi Machi 2024, ambao umesaidia katika ukuaji wa Huduma Jumuishi za Fedha nchini.
Aidha, aliisisitiza taasisi hiyo kuangalia namna ambayo inaweza kuboresha mfumo huo wa TIPS ambao unafanana na Mfumo wa Malipo wa Unified Payment Interface (UPI) unaotumika nchini India kwa ajili ya kustawisha uchumi wa nchi.
Kwa upande wa msimamizi wa maendeleo ya biashara Afrika, Bw. Nehal Sha, aliipongeza Benki Kuu na Serikali kiujumla kwa hatua iliyopiga katika maendeleo ya mifumo ya malipo na wameahidi kutoa ushirikiano katika kuboresha sekta hiyo.
Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za makao makuu ndogo ya BoT, Dar es Salaam, kilihudhuriwa pia na Naibu Gavana Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila Pamoja na wawakilishi kutoka Jumuiya ya Mabenki ya Tanzania (TBA), Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na taasisi zinazotoa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao.