Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) chawanoa Wanataaluma na Maafisa Waendeshaji wa Nelson Mandela katika eneo la kutoa Huduma za Ushauri wa Kitaalamu

ARUSHA-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kupitia Kurugenzi yake ya Huduma za Ushauri wa Kitaalamu, kinaendelea na mafunzo ya siku 5 ya Usimamizi wa zabuni na stadi za ushauri wa kitaalamu kwa wanataaluma na maafisa waendeshaji 21 wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST).Mafunzo hayo yalianza Jumatatu tarehe 3 na yatahitimishwa Ijumaa tarehe 7 Juni 2024. Mafunzo hayo yanafanyika katika Hoteli ya Corridor Springs jijini Arusha.
Kozi hiyo inaendeshwa na Prof. Deus Ngaruko na Bw. Augustino Kitulo (Wawezeshaji wa Ndani ya Chuo) kwa kushirikiana na Bw. Innocent Deus (Mwezeshaji wa Nje ya chuo).

Katika ufunguzi wa mafunzo hayo uliofanyika kupitia mtandao, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Utafiti na Ubunifu (DVC-RI) wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST),Prof. Anthony Mshandete alitoa shukrani kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kukubali kutoa mafunzo haya kwa wafanyakazi wa NM-AIST.
Aliwahimiza wafanyakazi waliohusishwa kuchangamkia fursa hii ili kuongeza utaalamu wao katika kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu, na hivyo kuongeza thamani yao katika eneo ili ambalo ni moja ya maeneo makuu matatu ya huduma za chuo kwa jamii.

Thamani hii itaimarisha zaidi uwezekano wa kuongeza kipato chao na cha chuo, pamoja na kuongeza umaili katika ufundishaji wa masomo na huduma nyingine za chuo kivitendo unaoendana na mahitaji ya soko.
Aidha, alitoa shukrani kwa Prof. Deus Ngaruko pamoja na wawezeshaji wengine na mkurugenzi anayehusika eneo hili, Dkt. Nfuka na Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania kwa ujumla kwa michango yao ya kina katika mafunzo haya.

Alisisitiza umuhimu wa kuanzisha ushirikiano endelevu kati ya Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, kwa lengo la kunufaisha vyuo hivi na taifa zima kwa ujumla.
Awali katika kuanza mafunzo haya, Mratibu wa huduma za Ushauri wa Kitaalamu katika Taasisi hii ya Nelson Mandela (NM-AIST), Dkt. Elizabeth Mkoba, alisema mpango huu wa mafunzo unalenga kuwajengea uwezo wafanyakazi kwa kuwapa ujuzi unaohitajika ili kutoa zaidi na kwa weledi huduma za ushauri wa kitaalamu.

Lengo sio tu kuongeza mapato ya taasisi, lakini pia mapato ya mtu mmoja mmoja na hivyo ustawi ulio bora wa wafanyakazi wake.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri wa kitaalamu kutoka Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania, Dk. Edephonce Nfuka, alisema lengo la chuo kikuu hicho ni kutoa mafunzo yatakayosaidia wataaluma na waendeshaji na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa ujumla kupata mapato na ubobezi zaidi kwa kushiriki katika miradi ya huduma za ushauri wa kitaalamu.
Kwa kupata ubobezi huu pia itawasaidia katika kutimiza vizuri zaidi na kwa vitendo na uhalisia ufundishaji na utekelezaji wa kazi za msingi kama vile kufundisha na kuimarisha mifumo ya kidigitali hivyo kuendana na mahitaji ya soko, jambo ambalo linasisitizwa na Sera Mpya ya Elimu na Kufundisha ya 2014 toleo la mwaka 2023 linalosisitiza elimu ujuzi.

Zaidi ya hayo, Mkurugenzi huyu ambaye pia ni mhadhiri wa Sayansi ya Kompyuta, alieleza kuwa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania kinaangalia uwezekano wa kuanzisha ushirikiano katika eneo hili na mengine na taasisi hii ambayo kimsingi eneo lake la kazi ni Afrika.

Wakati Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, pamoja na kuwa na wanafunzi ndani na nje ya nchi, ndio chuo kikuu pekee chenye vituo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa maana ya uwepo wa Vituo vya Uratibu Unguja na Pemba.
Uendeshaji wa mafunzo haya pia unajumuisha uratibu wa Revocutus Biro na Mwanuzi Babyegeya maafisa waendeshaji toka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news