DCEA na mikakati minne ya kulinusuru Taifa dhidi ya dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema, inaendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutekeleza kikamilifu mikakati yake minne ili kuhakikisha jamii ya Watanzania hususani vijana wanabaki salama bila dawa za kulevya.
Sara Ndaba ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii wa DCEA Kanda ya Kaskazini ameyabainisha hayo hivi karibuni katika mahojiano na Lumen TV kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya.

Kwa Kanda ya Kaskazini yanatarajiwa kuadhimishwa Juni 23,2024 katika Viwanja vya Mgambo (Gymkhana) vilivyopo jijini Arusha huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Paul Makonda,

Huku Kitaifa, maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika Juni 28 hadi 30,2024 katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza ambapo yanaongozwa na kauli mbiu ya "Wekeza kwenye Kinga na Tiba, Kudhibiti dawa za Kulevya".

Amesema,Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini wanafanya kazi kwa kuzingatia ile miongozo au mikakati ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya makao makuu ambayo kiujumla ilianza mwaka 2015 kupitia Sheria Na.5 ambapo taasisi hii ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

"Na tunatekeleza ile mikakati minne ambayo mkakati wa kwanza ni kuzuia uzalishaji na upatikanaji wa dawa za kulevya.

"Mkakati wa pili ni kuzuia ule uhitaji wa dawa za kulevya,mkakati wa tatu ni kupunguza madhara ya dawa za kulevya na mkakati wa nne ni kuimarisha ushirikiano wa Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

"Kwa hiyo, hiyo ni mikakati yetu minne ambayo tunaitekeleza na hata tulipoletwa huku Kanda ya Kaskazini mwezi Septemba,mwaka jana ni hiyo mikakati tunaenda nayo.

"Kwa hiyo tunadhibiti dawa za kulevya, upatikanaji lakini pia tunatoa elimu katika makundi mbalimbali kupitia Muongozo wa Utoaji wa Elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya."

Naye Afisa Elimu Jamii wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini, Shaban Miraji amesema,taasisi hiyo imefanikiwa kutoa elimu kwa makundi mengi na tangu waanze kutoa huduma katika kanda hiyo wamepata mafanikio makubwa.

"Tumeendesha operesheni mbalimbali za kukamata wahalifu wa dawa za kulevya. Lakini pia na wakulima, tumeenda kule Kisimiri tumefanya operesheni mbalimbali na sasa hivi hali ni shwari kabisa.

"Watu ambao wapo Kisimiri sasa hivi wanajishughulisha na kilimo cha karoti, maharage na mazao mengine ya chakula. Wapo wachache ambao wanaendelea na kilimo cha bangi hususani wale ambao wanalima katika maeneo ambayo ni ya hifadhi,"amesema huku akibainisha hao pia operesheni mbalimbali zitawafikia huko walipo.

Kwa nini DCEA?

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015.

Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995.

Ni ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news