DODOMA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko ameipongeza Mamalaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuendelea kutoa huduma bora za hali ya hewa nchini.
Amesema hayo Juni 3,2024 wakati alipotembelea banda la TMA kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yanayofanyika katika viwanja vya JICC jijini Dodoma.
Dkt. Biteko alikuwa mgeni rasmi wa ufunguzi wa maadhimisho hayo muhimu kwenye ukuaji wa sekta ya mazingira nchini na alitembelea banda la TMA na kupokelewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt. Ladislaus Chang’a.
“Hongereni sana kwa huduma bora za utabiri mnazotoa kila siku na zinatusaidia sana, hongereni sana,”amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake,Dkt. Chang’a aliwaomba wananchi wa Dodoma na wale wa mikoa ya jirani watumie fursa hii kwa kutembelea banda la TMA kwenye maadhimisho haya ili kujifunza masuala mbalimbali ya mazingira na masuala mbalimbali ya hali ya hewa na huduma zitolewazo na TMA.
“Karibuni wananchi wote katika banda la TMA, mje kujifunza na kuongeza uelewa wa huduma za hali ya hewa na matumizi yake katika sekta zote za kiuchumi na kijamii. Kujifunza uhusiano wa hali ya hewa na mazingira yanayotuzunguka. Tunao wataalam bingwa wa hali ya hewa na wapo tayari kutoa elimu,” amesema Dkt. Chang’a.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inashiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya wiki ya Mazingira kwa mwaka 2024 yenye kauli Mbiu "Urejeshwaji wa Ardhi, Ustahimilivu wa Hali ya Jangwa na Ukame."
Tags
Doto Biteko
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Siku ya Mazingira Duniani
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
TMA Tanzania