Elimu ya Fedha ni endelevu nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha, Mheshimiwa Dkt.Mwingulu Lameck Nchemba amesema, wizara inaendelea kupokea maoni na mapendekezo mbalimbali kutoka kwa wadau kuhusu umuhimu wa elimu ya huduma za fedha kwa umma katika kukuza shughuli za kiuchumi na ustawi wa jamii.
Dkt.Nchemba ameyasema hayo leo Juni 4, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/2025.

Amesema, kwa mwaka 2023/24, wizara imeanza kutekeleza Mkakati wa Utoaji wa Elimu ya Fedha Vijijini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Elimu ya Fedha kwa Umma ya Mwaka 2021/22-2025/26.

"Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na taasisi za usimamizi ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima,

"Mamlaka ya Masoko ya Mitaji Dhamana pamoja na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imeunda timu maalumu ya wataalamu kutoa elimu kwa umma, hususanI vijijini.

"Ni kwa utaratibu wa semina, warsha, makongamano, filamu, runinga, redio, mitandao ya kijamii na mafunzo kwa waratibu waliopo katika halmashauri zetu,"amesisitiza Waziri Dkt.Nchemba.

Dkt.Nchemba amesema,makundi yaliyopewa kipaumbele katika zoezi hilo linaloendelea la elimu ya fedha kwa umma ni wajasiriamali wadogo, wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalumu na waajiriwa.

"Kwa kuwa ni makundi yaliyoathirika zaidi na mikopo ijulikanayo kama kausha damu. Maeneo yaliyofikiwa hadi sasa ni halmashauri za mikoa ya Singida, Manyara na Kagera.

"Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, elimu ya fedha kwa wananchi wetu ni zoezi endelevu, hivyo, elimu itaendelea kutolewa na kuboreshwa kulingana na mazingira, mahitaji na maoni ya wadau.

"Aidha, kwa kuwa sisi wabunge ni sehemu ya jamii, tunaweza kutembelea mtandao wetu wa elimu ya fedha kwa umma kupitia https://www.youtube.com/@MofURT au HAZINA TV kupata elimu ya fedha, na muhimu zaidi kuwa mabalozi wetu wa elimu ya fedha kwa umma."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news