Elimu ya Fedha yawafikia wajasiriamali wadogo Sumbawanga

NA EVA NGOWI

SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha itaendelea kuwashauri wananchi kwa ujumla kushiriki kwa wingi katika semina zinazoendelea kutolewa kuhusiana na elimu ya fedha ili kuepukana na mikopo umiza ama mikopo kausha damu.
Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha- Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro,akitoa elimu ya fedha kwa Wajasiriamali wadogo wadogo (hawamo pichani) katika Ukumbi wa Manispaa ya Wilaya ya Sumbawanga mjini mkoani Rukwa.

Hayo yamesemwa na Bw. Salim Kimaro, Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha- Wizara ya Fedha, wakati wa Semina na Wajasiriamali wadogo iliyofanyika katika kumbi za Manispaa Wilaya ya Sumbawanga Mjini Mkoani Rukwa kwa kuwahimiza wananchi wote popote pale walipo waendelee kutufuatilia na kuhudhuria katika maeneo ambayo yatafanyika semina hizo ili waweze kujipatia elimu ya fedha kwa mustakabali wa uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Bw. Kimaro alisema malengo ya elimu ya fedha kwa wananchi ni kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kupata na kutumia huduma za fedha hapa nchini.
Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha- Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, (wa kwanza kulia) akielezea malengo ya utoaji elimu ya fedha kwa wajasiriamali wadogo mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Manispaa ya Sumbawanga ambapo timu ilipokelewa na Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu aliyekaa meza kuu, Bw. Donatus Wegina.

Alisema kuwa,huduma hizo ni suala ambalo linapaswa kufahamika katika matumizi yake na upatikanaji wake ili kuwaepusha wananchi na changamoto mbalimbali zinazotokana na kutoelewa masuala mbalimbali ya elimu ya fedha na kujiepusha na mikopo kausha damu.

“Tumekuja Mkoa wa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga Mjini kwa ajili ya uendelevu wa zoezi letu la kutoa elimu ya fedha kwa umma, zoezi ambalo litafanyika katika mikoa nane katika awamu hii na mikoa mingine yote itafuata hadi wananchi wote watakapofikiwa," amesema Bw. Kimaro.
Akizungumza wakati wa semina hiyo alisema Changamoto nyingi zinatokana na uelewa mdogo wa elimu ya fedha na hasa katika masuala ya mikopo ambapo alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kufahamu kuwa kabla ya kukopa ni muhimu kuwa na malengo ya kukopa, kufahamu vyema watoa huduma watakao kwenda kukopa kama wamesajiliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni lakini pia, ni muhimu kusoma na kuelewa mikataba ya watoa huduma ili wasije ingia katika matatizo ya mikopo kausha damu.

Bw. Kimaro aliongeza kuwa matarajio ya kutoa elimu hiyo ni kuwapata wananchi wenye weledi katika masuala ya fedha na hivyo kuepuka kujiingiza katika biashara zisizo halali katika masuala ya fedha lakini kubwa zaidi ni kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba, kuwekeza katika maeneo yenye tija na kukopa mahali palipo salama lakini pia kupanga mipango sahihi ya maisha baada ya kustaafu.

Awali akizungumza katika semina hiyo Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Bi. Tabu Rajab Hessein, aliwashukuru Watumishi wa Wizara ya Fedha, Watumishi wa Manispaa ya Sumbawanga pamoja na washiriki yaani wajasiriamali wadogowadogo kwa ujumla wao na kusema kuwa elimu waliyoipata watakwenda kuifanyia kazi.
Baadhi ya Wajasiriamali wadogo wakisikiliza elimu ya fedha inayotolewa na mtaalamu wa Wizara ya fedha kutoka Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha, Bw.Salim Kimaro.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha).

“Mimi binafsi nimejifunza kwa sababu mengi yaliyokuwa yanaoneshwa kwenye video, wanawake wengi yanatugusa kwa namna moja ama nyingine. Wanawake tulio wengi tuko kwenye vikoba lakini hatujui vikoba vile utaratibu wa kisheria ukoje,”amesema Bi. Tabu.

Aliongeza kuwa malengo ya elimu hiyo ni kuwawezersha wakinamama pamoja na akina baba kwenda kwenye Taasisi za kifedha au kwenye vikoba ambavyo vimesajiliwa na vinatambulika kisheria ili hata kukitokea shida ni rahisi mtu kufuatilia haki yake na akaipata,” amesema Bi.Tabu Hussein.

Akizungumzia umuhimu wa semina hiyo, Bi. Janerosa Schilian, kutoka Kata ya Chanji ambaye ni mfanyabiashara mdogo alisema amejifunza vitu vingi ikiwemo nidhamu ya pesa.

“Nimejifunza katika biashara zangu inawezekana ningekuwa mbali sana, kwa sababu ya utovu wa nidhamu ya pesa, ndio maana yamkini maisha yangu yako chini, lakini nimejifunza kwamba ninapukuwa nikipata pesa natakiwa nizipangie bajeti mimi na familia yangu nisiingize mambo mengine ambayo yalikuwa hayajapangiwa bajeti,”amesisitiza Bi. Schilian.

Elimu ya Fedha ni programu inayotolewa kwa kuzingatia Mwongozo wa Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ambao ni wa miaka kumi. Mwongozo huo ambao pamoja na mambo mengine ni lazima wananchi wapate elimu ya fedha katika makundi mbalimbali kama vile Vyama vya Ushirika, Wanafunzi, Waalimu, Wafanyakazi, Vikundi vya huduma ndogo za fedha na Wananchi kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news