Elimu ya Fedha yawafikia wananchi Shinyanga

NA ASIA SINGANO
WF

WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga, wamepata fursa ya kujifunza elimu ya fedha kuhusu uwekezaji, matumizi sahihi ya fedha binafsi, utunzaji wa fedha binafsi, mambo ya kuzingatia kabla ya kuchukua mikopo, faida ya kuwekeza kwa ajili ya maisha ya uzeeni na kustaafu ili kufanya maamuzi sahihi wanapotumia huduma za fedha na kukuza uchumi.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akitoa ufafanuzi kuhusu filamu ya elimu ya fedha iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha kabla ya kuwawekea wananchi wa kata ya Iselamagazi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, filamu hiyo yenye maudhui kuhusu umuhimu wa kuweka akiba, matumizi sahihi ya fedha na utunzaji wa fedha binafsi, uwekezaji sehemu sahihi na salama, mambo ya kuzingatia wakati wa kukopa.

Akizungumza kuhusu maeneo yatakayofikiwa katika mkoa wa Shinyanga, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kupata elimu ya fedha kutokana na umuhimu wa elimu hiyo katika kukuza uchumi wa wananchi na nchi kwa ujumla.

‘’Wizara ya Fedha inaendelea na kutoa elimu ya fedha, na kwa sasa tupo katika Mkoa wa Shinyanga, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, baada ya hapa tutaelekea katika Wilaya nyingine za Msalala, Ushetu pamoja na Kahama, hivyo tunatoa wito kwa wananchi maeneo ambayo tutapita wajitokeze kwa wingi.’’
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo, akizungumza na watalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na watumishi wengine wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, walipofika ofisini kwake kumweleza lengo la ujio wao na maeneo wanayotarajia kutoa elimu ya fedha katika Mkoa huo.
Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akimkabidhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Pro. Siza Tumbo, Nyenzo ya kufundishia elimu ya fedha, walipofika ofisini kwake kujitambulisha.

Awali, kabla ya mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Anamringi Macha, aliwataka wananchi wa Mkoa wake kushiriki vyema katika mafunzo hayo kutokana na wananchi wengi mkoani humo kujihusisha na mikopo bila kuzingatia malengo hali inayosababisha kupata migogoro ya kifamilia mpaka kupoteza mali zao.

“Jamani! Watu wanaandikishwa kwenye mikopo bila mpangilio, utasikia niandikishe hata kabla hajajua mkopo una riba kiasi gani, akisikia tu kuna gari inatoa mikopo hapa kabla hajafika anapiga simu niandikishe anachukua mkopo bila malengo kwahiyo watumie elimu hii kama fursa,’’ alisisitiza Bw. Macha.
Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akizungumza kwa niaba ya wataalamu wa kutoa elimu ya fedha (hawapo pichani), kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), baada ya wataalamu hao kufika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Anamringi Macha, kabla ya kuelekea Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mkoani Shinyanga kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi.
Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Anamringi Macha, nyenzo ya kufundishia elimu ya fedha, mara baada ya kuwasili katika Mkoa wa Shinyanga ambapo baada ya zoezi hilo, timu ya wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakiambatana na Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa walielekea katika Kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kutoa elimu ya fedha.

Kwa upande wake Bi. Anastazia Elias mmoja wa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga aliyeshiriki mafunzo ya elimu ya fedha, alisema elimu ya fedha kwake ni jambo geni na anaipongeza Wizara ya Fedha kwa kumfungua macho katika suala zima la kuweka akiba na matumizi ya fedha kwa ujumla huku akiomba zoezi hilo liwe endelevu.

“Mimi kwanza sijawahi kuona lakini nimeona leo, elimu ya fedha imenipa mwanga mkubwa sana, maana maisha yetu tulikuwa tunayaendesha kibubu, hii huduma iendelee kutolewa zaidi maana sisi wanawake unakopa laki moja unafika nyumbani alfu thalathini yote imeisha kabla ya malengo uliyokopea.’’

Naye Buhohela Shija, alisema kuwa kabla ya mafunzo hayo wananchi wengi hawakuwa na uelewa kwenye masuala ya fedha hivyo elimu hiyo ni vyema ikaendelea kutolewa kwa wananchi wote.

“Natoa shukrani zangu za dhati kwa ugeni huu wa Wizara ya Fedha kuja kutuletea elimu stahiki tumejifunza vya kutosha kuhusu uwekaji akiba maana watu wengi hatuna hiyo elimu.’’ 
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Anamringi Macha (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha wakishirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakiongozwa na Afisa Usimamizi wa Fedha Kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava (watatu kushoto), Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Mwile Kauzeni (watatu kulia), pamoja na Maafisa wengine kutoka Wizara ya Fedha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Baadhi ya wajasiriamali na wananchi wa kata ya Iselamagazi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, wakipata elimu ya fedha kwa njia ya filamu yenye maudhui kuhusu matumizi sahihi ya fedha, umuhimu wa kupanga bajeti na kuitekeleza, umuhimu wa kusajili vikundi vya huduma ndogo za fedha (Vikoba), utunzaji wa fedha binafsi, umuhimu wa kushirikisha familia na watu wa karibu kwenye masuala ya fedha na uwekezaji, umuhimu wa kukata bima ya biashara na mali nyingine, filamu hiyo imeandaliwa na Wizara ya Fedha lengo likiwa ni kusambaza elimu ya fedha kwa njia rahisi ya burudani ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa masuala ya huduma za fedha.
Picha za matukio mbali mbali ya mafunzo ya elimu ya fedha katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga, elimu hiyo ya fedha ilianza kutolewa maeneo ya mijini kupitia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kwa Mikoa ya Dar Es Salaam, Mwanza na Arusha, ambapo kwa sasa programu hiyo imejikita kuwafikia wananchi wote kwa lengo la kuwaongezea uelewa wa masuala ya fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika mahitaji na matumizi ya Huduma za Fedha maeneo mengine yaliyofikiwa ni pamoja na Mkoa wa Manyara, Singida, Kagera, Rukwa, Kigoma, Tabora, Simiyu na sasa ni zamu ya Mkoa wa Shinyanga. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha-Shinyanga).

Wizara ya Fedha itaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa Mikoa yote nchini kwa kuwa ni moja ya mpango wake wa kuhakikisha wananchi wote wanapata uelewa kuhusu huduma za kifedha ikiwemo masuala ya akiba, mikopo na uwekezaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news