NA EVA NGOWI
SERIKALI imetoa rai kwa wananchi kuepuka kukopa fedha kwenye vikundi vinavyotoa huduma za kifedha bila kusajiliwa rasmi kwa mujibu wa sheria ili kuepuka athari zinazoambatana na mikopo umiza.
Wajasiriamali kutoka kijiji cha Kaengesa Wilaya ya Sumbawanga vijijini, wakisikiliza semina ya elimu ya fedha kutoka kwa mtaalamu wa Wizara ya Fedha Bw. Jackson Mushumba.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Msimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Jackson Mshumba, wakati wa semina ya masuala ya fedha iliyofanyika katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Bi. Everanda Kastoma (kushoto) kutoka Kijiji cha Minazi AMCOS, Wilaya ya Sumbawanga, akipokea zawadi ya fulana kutoka kwa Bw. Jackson Mushumba (kulia) Afisa Msimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha.
“Tumekuja kubaini kwamba wananchi wengi wako katika vikundi ambavyo havijasajiliwa rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha ya mwaka 2018, kwa hiyo nitoe rai kwa wananchi ni vyema wakawa na mwamko wa kujiunga katika vikundi ambavyo ni rasmi na vimesajiliwa kwa mujibu wa Sheria hiyo,"alisema Bw. Mshumba.
Baadhi ya Wanavikundi katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Makao Makuu- Laela, wakisikiliza semina ya mafunzo ya Elimu ya Fedha yaliyotolewa na Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha – Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro.
Bw. Mshumba alisema kuwa Serikali inaendelea na programu hii ya utoaji elimu vijijini hususan kwa Mkoa wa Rukwa, ambapo wananchi wamepata elimu namna wanavyoweza kuwa na nidhamu ya kujiwekea akiba lakini pia wamepata uelewa juu ya mikopo umiza ili kuepukana na changamoto hii kwa sasa ya mikopo kausha damu.
Alisema kuwa katika mwendelezo wa zoezi hilo imebainika kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa masuala ya mikopo, taratibu za mikopo hawazifahamu lakini pia wananchi wengi hawafahamu masharti yaliyoko katika mikopo wanayochukua kwa watoa huduma mbalimbali.
Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, akitoa elimu ya fedha kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Rukwa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kanisa la Moravian Wilaya ya Sumbawanga Mjini.
Bw. Mshumba aliongeza kwa kuwasisitiza wananchi kuwa kabla ya kuchukua mikopo ni vyema wakajiridhisha kuhusu suala la riba, kama mtoa huduma amesajiliwa kwa mujibu wa sheria na pia waelewe vigezo na masharti yaliyopo kwenye mkataba husika.
Baadhi ya Wanavikundi katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Makao Makuu- Laela, wakifuatilia filamu inayoelezea mafunzo ya Elimu ya Fedha.
Alitoa rai kwa wananchi kwa kuwaomba endapo watabaini kwamba kuna vikundi vidogo vya huduma ndogo ya fedha vipo mitaani na havijasajiliwa watoe taarifa kwa mamlaka husika ambazo ni pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye mamlaka zao za Wilaya na Mikoa.
Awali, akizungumza katika semina hiyo Mkazi wa Kijiji cha Kaengesa, Wilaya ya Sumbawanga vijijini, Bi. Rehema Lukali, alisema kuwa ujio wa Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha umewafungua macho kuhusiana na akiba, kwamba ili uaminike katika vyombo vya kifedha lazima mtu awe mwanachama na chama chake kiwe kimesajiliwa kisheria.
Afisa Uwezeshaji -Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi, Bw. Omari Haji Bakari akitoa elimu ya fedha kwa wajariamali wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Makao Makuu- Laela.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha).
Aidha, Bw. Mishek Kassian ambaye pia ni mwana kikundi kikundi cha Kambarage kilichopo katika kijiji cha Lyapona, Wilaya ya Sumbawanga, alisema kuwa kupitia elimu aliyoipata amejifunza mengi na ataenda kuwaelimisha watu wengine maana anaona mikopo mingi inakopeshwa na watu binafsi na taasisi mbalimbali ambapo wengi wanakopa bila kuwa na malengo.