MWANZA-Watumishi wanne katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza wamefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela kwa tuhuma za kufanya ubadhirifu wa fedha za mapato.
Juni 24,2024 watumishi hao ambao ni maafisa uchumi, wahasibu na maafisa uvuvi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wamefikishwa mahakamani hapo kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka.
Sambamba na ufujaji na ubadhirifu wa shilingi nilioni 67 kinyume na vifungu vya 28(2),(3) na 31 vya PCCA sura ya 329 na marejeo yake ya mwaka 2022.
Mashauri manne dhidi ya watumishi hao wa Serikali yamefunguliwa mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi,Mhe.Christian Mwalimu wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, na yamesomwa Mahakamani na waendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wakili Jovine Majura na Hilal Nikitas.
Washtakiwa hao kwa nyakati tofauti kati ya Julai 1, 2020 hadi Juni 30,2021 wanadaiwa kutenda makosa hayo.
Inadaiwa wakiwa na nia ovu walitumia madaraka yao vibaya na kushindwa kuwasilisha fedha za mapato ya Serikali zaidi ya shilingi milioni 67 kwenye akaunti ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Mapato hayo ni makusanyo mbalimbali ya fedha za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Kitendo cha kutokuwasilisha Benki fedha hizo za Serikali ni kinyume na kifungu cha 50(5) ya Memoranda ya Fedha za Halmashauri za mwaka 2009, ambazo kimsingi walijipatia manufaa binafsi.
Watumishi waliofikishwa mahakamani ni Hellen Mcharo ambaye ni Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mwenye kesi namba 17146/2024.
Mwingine ni Medard Chenyambuga ambaye ni Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Manispaa mwenye kesi namba 17147/2024.
Pia, Speratus Cosmas ambaye ni Mhasibu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mwenye kesi namba 17148/2024.
Akiwemo Winning Temu ambaye ni Mhasibu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mwenye kesi namba 17149/2024.
Washtakiwa wote wamekana makosa yao na wawili wapo nje kwa dhamana na wawili wako rumande kwa kushindwa kukidhi vigezo vya dhamana.
Kesi hizo zitakuja tena mahakamani Julai 4 na Julai 18, 2024 kwa ajili ya hoja za awali.
Tags
Habari
Mahakamani Leo
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania
Watumishi wa Umma