NA GODFREY NNKO
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele amesema, makundi yote wakiwemo wazee, wajawazito na watu wenye ulemavu wamewekewa utaratibu mzuri wa kushiriki katika zoezi la maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga nchini.
Jaji Mwambegele ameyasema hayo leo Juni 12,2024 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa tume na wahariri wa vyombo vya habari ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
"Tume imeweka utaratibu mzuri wa kuyahudumia makundi yote wakati wa maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura."
Pia, Jaji Mwambegele amewaomba wahariri kutumia vyombo vyao vya habari kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo ambalo uzinduzi rasmi unatarajiwa kufanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa siku ya Julai Mosi, 2024 mkoani Kigoma.
Maboresho ya mwisho yalifanyika mwaka 2019 na mwaka 2020 huku uandikishaji huu wa wapiga kura utahusisha uchukuaji wa alama za vidole vya mikono, picha na saini na kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya wapiga kura.
"Kwa mujibu wa Kifungu cha 16 (5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024 uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utakuwa mara mbili kati ya kipindi kinachoanza mara baada ya uchaguzi mkuu na kabla ya siku ya uteuzi."
Aidha,wanaohusika katika zoezi hilo ni wananchi ambao wametimiza umri wa miaka 18 na kuendelea ambao hawakuandikishwa hapo awali.
Pia, wananchi watakaotimiza miaka 18 kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na waliojiandikisha awali na wamehama kata au jimbo moja kwenda jingine.
Vile vile, kwa waliopoteza sifa mfano wale waliofariki wataondolewa katika daftari huku wenye taarifa zilizokosewa wakati wa uandikishaji na waliopoteza au kadi zao kuharibika watahudumiwa.
Kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Daftari hilo linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638 kutoka 29,754,699 ya mwaka 2020 hilo ni ongezeko la wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7.
Aidha, katika zoezi hilo wapiga kura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wataondolewa katika daftari kwa kupoteza sifa za kuwa wapiga kura.