Hausigeli, kamwe usimdharau

NA LWAGA MWAMBANDE

WASAIDIZI wa ndani (house girls) ni miongoni mwa watu muhimu katika familia na maisha yetu ya kila siku.
Picha na The Star.

Umuhimu wao si tu kwa sababu wanatusaidia kutekeleza baadhi ya shughuli ndogo ndogo nyumbani bali pia ni wasimamizi wa makazi na watoto, pindi Baba na Mama wanapokwenda kutekeleza majukumu yao ya kuipatia familia riziki ya kila siku.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa,kadri utakavyomkarimu msaidizi wako wa ndani kama unavyofanya kwa watoto wako, tegemea baraka nyingi kutoka kwa Mungu.Endelea;

1. Housegeli ni lango, kamwe usimdharau,
Kashikilia mlango, umtunze angalau,
Usimlishe matango, wewe ukila pilau,
Huo uponyaji wako, uko mikononi mwake.

2. Hausigeli mtoto, naye mpe kaukau,
Simtenge na watoto, hata akajidharau,
Na yeye ataka joto, wala usimsahau,
Huo uponyaji wako, uko mikononi mwake.

3. Akutunzia watoto, hebu mpe lake dau,
Nyumbani pana fukuto, wewe usiwe Bi Chau,
Muonye kama mtoto, wala hatakudharau,
Huo uponyaji wako, uko mikononi mwake.

4. Hausigeli twasoma, ni kweli sio nahau,
Kwa Naamani mkoma, nyumbani hakusahau,
Kunapatikana mema, kumponya angalau,
Huo uponyaji wako, uko mikononi mwake.

5. Hausigeli kwa wema, kashauri bila dau,
Ya kwamba baba mkoma, kwao asikidharau,
Akaombewe kwa wema, ukoma ausahau,
Huo uponyaji wako, uko mikononi mwake.

6. Naamani kaondoka, sio kumfwata Njau,
Ni kwa mtu wa Rabuka, amtibu angalau,
Ukoma ukabanduka, hata akausahau,
Huo uponyaji wako, uko mikononi mwake.

7. Kasikiza kijakazi, bila ya kumdharau,
Akaponywa ile ngozi, ugonjwa akasahau,
Wangekuwa ni washenzi, singewaambia au?
Huo uponyaji wako, uko mikononi mwake.

8. Hivi wangapi wazazi, waliojaa dharau,
Hausigeli walezi, vile wanawadharau,
Pamoja na yao kazi, wawanyima lao dau?
Huo uponyaji wako, uko mikononi mwake.

9. Mbona nyumba yako yote, atunza wamsahau?
Wampa shughuli zote, unachelewesha dau?
Na hao watoto wote, waache wamdharau?
Huo uponyaji wako, uko mikononi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news