DODOMA-Makamu wa Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa ufanisi mkubwa wa kazi ya kutoa huduma za hali ya hewa, zinazosaidia sekta za kiuchumi na kijamii nchini.
Ameyasema hayo Juni 5,2024 alipotembelea banda la TMA kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani, yanayo fanyika katika viwanja vya JICC jijini Dodoma.
Dkt. Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho haya muhimu, Alitembelea banda la TMA na aliambatana na Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, na Waziri wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Selemani Jafo.
“Hongereni sana Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, na kama nilivyosema mwanzo, tunaona utofauti mkubwa sana, ufanisi wenu wa kazi umeongezeka, tunaona matunda ya uwekezaji ambao serikali imefanya kwani taarifa zenu zina uhakika,”amesema Dkt. Mpango.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia nchi, Dkt.Ladislaus Chang’a aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mwendelezo wa uwekazaji unaoendelea kufanya kwenye sekta ya hali ya hewa nchini.
“Napenda kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji wa mkubwa unaoendelea kufanywa kwenye sekta yetu ya hali ya hewa nchini.
"Ndani ya miaka mitatu Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa wa maendeleo kwenye sekta ya hali ya hewa kupita nchi zote za Afrika Mashariki na Kati. Mpaka mwanzoni mwa mwaka ujao tutakuwa na Rada saba za hali ya hewa,”amesema Dkt Chang’a.
Tags
Dr Philip Isdory Mpango
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)