NA GODFREY NNKO
JULAI Mosi,2024 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua rasmi zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele uzinduzi huo utafanyika rasmi mkoani Kigoma.
Vile vile, siku ya uzinduzi ndiyo siku ambayo pia uboreshaji utaanza katika Mkoa wa Kigoma, Katavi, Tabora, Kagera na Geita na baadaye mikoa mingine.
Ili kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, tume inatarajia kutekeleza zoezi hilo katika awamu ya kwanza kupitia mizunguko 13 kadri itakavyokuwa ikitoa ratiba.
Aidha, kupitia mikutano na wadau mbalimbali iliyoanza Juni 7, 2024 ambapo tume imekuwa ikikutana nao wakiwemo waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, viongozi wa tume wamebainisha kuwa,
Katika uboreshaji huo kutakuwa na mifumo miwili ukiwemo Mfumo Mkuu wa VRS (Voter Registration System) na Mfumo Saidizi wa OVRS (Online Voter Registration System).
VRS ni mfumo ambao umekuwa ukitumika katika mazoezi ya uboreshaji wa daftari uliotangulia ikiwemo mwaka 2015 na 2020.
Huku, OVRS ni mfumo ambao tume imeuanzisha kwa lengo la kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi kwa njia ya mtandao.
Kwa mujibu wa INEC, mifumo yote miwili itahusisha matumizi ya fomu tatu za uandikishaji kama ilivyokuwa katika mazoezi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura miaka ya 2014/15 na 2019/20.
Fomu Namba 1 itahusika kuandikisha wapiga kura wapya, Fomu Namba 5A ni kwa wanaoboresha taarifa zao, wanaohama vituo, waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika.
Wakati huo huo, Fomu Namba 5B ni kwa ajili ya kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwepo katika Daftari la Wapiga Kura nchini.
INEC imebainisha kuwa, mifumo yote miwili inahusisha matumizi ya Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) ambayo huwa inatolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Aidha, mifumo hiyo ya uandikishaji ya INEC inaweza kuvuta taarifa za NIDA iwapo mpira kura atakuwa na NIN, hivyo kurahisisha zoezi la uandikishaji ingawa namba hiyo si hitaji la lazima ili mpiga kura kujiandikisha.
Akiwasilisha mada yake kwenye mikutano hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,Bw.Ramadhani Kailima amesema, uboreshaji wa daftrai pamoja na mambo mengine utahusu kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Ameongeza kuwa zoezi hilo pia Iitatoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walioandikishwa awali.