INEC yatoa ombi kwa viongozi wa dini kuelekea maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele amewaomba viongozi wa dini nchini kuwahamasisha waumini wao ili waweze kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini.
Ni zoezi ambalo linatarajiwa kuanza Julai 1, 2024 ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa anatarajiwa kulizindua rasmi mkoani Kigoma.
Jaji Mwambegele ametoa ombi hilo leo Juni 10,2024 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa tume na viongozi wa dini ambao unaangazia kuhusu maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini.

"Hivyo tunawasii na kuwaomba mtumie fursa hizo wakati wa ibada kuwahamasisha wananchi ili waweze kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura."

Amesema, kwa mujibu wa Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, pamoja na majukumu mengine imeipa INEC jukumu la kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais, wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na madiwani kwa Tanzania Bara.

"Jukumu hilo pia, limeainishwa kwenye kifungu cha 16 (5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani Na.1 ya mwaka 2024 ambacho kinaweka sharti kwa tume kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu uliomalizika na kabla ya siku ya uteuzi wa wagombea kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaofuata."
Katika zoezi hilo, tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya raia wa Tanzania, kutoa fursa kwa wapiga kura ambao wamehama vituo kuboresha taarifa zao, wapiga kura kurekebisha taarifa zao, kupewa kadi mpya kwa waliopoteza au kuharibika.

Vile vile kuondoa wapiga kura ambao wamefariki na waliokosa vigezo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini.
Ameeleza, maboresho hayo yanatarajiwa kutumia teknolojia ya kisasa ikiwemo matumizi ya vishikwambi ili kuongeza ufanisi katika zoezi hilo.

Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amewashukuru viongozi wa dini kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiuonesha kwa tume kila wakati wanapotekeleza majukumu yao huku nayo ikiwaahidi ushirikiano zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news