INEC:Unaweza kuhama kituo kwa kutumia simu au kompyuta yako, jiandae maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

NA GODFREY NNKO

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema, imeboresha mfumo wa uandikishaji ambao kwa mara ya kwanza utamwezesha mpiga kura aliyepo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zake.
Aidha,mpiga kura anaweza kuhama kituo kwa kutumia simu au kompyuta na baadae kutembelea kituo anachokusudia kujiandikisha ili apatiwe kadi yake ya mpiga kura.

Hayo yamesemwa leo Juni 13,2024 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano kati ya tume na waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari nchini.
Mkutano wa leo ni mwendelezo wa mikutano mfululizo kati ya tume na wadau mbalimbali nchini ili kuwapa uelewa waweze kutoa elimu kwa wananchi waweze kushiriki katika maboresho ya daftari.

Aidha, mikutano hiyo ambayo ilianza Juni 7, mwaka huu inatarajiwa kuendelea mikoa yote ya Tanzania Bara kadri ratiba itakavyoruhusu.

Jaji Mwambegele amesema, kwa mujibu wa Kifungu cha 9 (1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya mwaka 2024, uboreshaji wa Daftari utahusu watu wote wenye sifa za kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
"Wakati wa zoezi hilo,tume imeweka utaratibu kwa watu wenye ulemavu, wazee,wagonjwa, wajawazito na wakina mama wenye watoto wachanga watakaokwenda nao vituoni kupewa fursa ya kuhudumiwa bila kupanga foleni."

Amewaomba makundi tajwa kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha au kuboresha taarifa zao vituoni kwa kuwa utaratibu mzuri wa kuwahudumia umewekwa.

Amesema, uboreshaji huo ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Julai Mosi, 2024 mkoani Kigoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Kassim Majaliwa kama ilivyokuwa uboreshaji wa mwaka 2015 na 2020 utahusisha matumizi ya teknolojia ya Biometric Voters' Registration (BVR).

"Mfumo wa teknolojia hii ya BVR hutumika katika kutambua mtu na kumtofautisha na mwingine. Uandikishaji huu wa wapiga kura utahusisha uchukuaji alama za vidole vya mikono,picha na saini na kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya wapiga kura."
Jaji Mwambegele amesema, tume inatarajia ushirikiano mkubwa kwa waandishi wa habari katika kuripoti kwa weledi kuhusu zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news